Na: Mwandishi Wetu, Michuzi TV
TAASISI ya Mama Ongea na Mwanao ikiongozwa na Mwenyekiti wake Steve Mengele maarufu Steve Nyerere imewatembelea na kuwapa pole waathirika wa mafuriko ya matope yaliyotokea Hanang mkoani Manyara na kusababisha maafa, majeruhi na uharibifu wa mali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Desemba 15, 2023 na Steve Nyerere ameeleza taasisi hiyo imeanza rasmi ziara yake katika mkoa huo na wameanza kwa kuwatembelea waathirika hao na kuwapa mkono wa pole.
Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao baada ya kufika Hanang wametembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara ambapo baadhi ya waathirika hao wanaendelea kupatiwa huduma za afya hapo ambapo kuna waathirika katika wodi ya wanaume,wanawake na watoto.
Kwa mujibu wa taasisi hiyo imefafanua inatambua mazingira magumu ambayo wanapitia waathirika wa mafuriko hayo , hivyo wameona iko haja ya kuwatembelea, kuwapa pole na kuwashika mkono.
Baadhi ya waathirika wa mafuriko hayo wameishukuru Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao kwa kuwatembelea na kuwapa pole wakiwa katika hospitali hiyo wakipatiwa huduma za matibabu.
Sambamba na hilo wameendelea kutoa shukrani zao kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa kuendelea kuwahudumia kuanzia mwanzo mpaka hivi sasa.