Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, Akizungumza leo Novemba 28, 2023 kwenye Kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodaus Balile akizungumza katika kikao kazi cha Msajili wa Hazina na Wahariri wa Habari kilichofanyika leo Novemba 28,2023 Jijini Dar es Salaam.
Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu, (kulia), akiagana na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodaus Balile (kushoto), mara baada ya kumalizika kwa Kikao kazi hicho Jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania TEF, Anitha Mendoza akishiriki kwenye Kikao kazi hicho.
(PICHA NA: HUGHES DUGILO)
Na: Mwandishi wetu, DAR ES SALAAMÂ
Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina inatarajia kufanya maboresho ya sheria ambazo zitasaidia sekta za umma kufanya kazi kwa ufanisi na kuleta tija katika utendaji.
Akizungumza leo Novemba 28, 2023 kwenye Kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema kuwa wakati umefika kwa wakurugenzi wa mashirika ya umma kufanya kazi kwa weledi katika kuhakikisha wanapata mafanikio katika utendaji wao.
“Ili mashirika ya umma yapige hatua yanapaswa kutoingiliwa katika utekelezaji wa majukumu yake, kuwekeza rasilimali fedha katika kufanikisha mipango mbalimbali ya maendeleo, pamoja na kuwekeana malengo na wasimamizi katika kufikia viwango vya mafanikio ndani ya muda fulani” amesema Mchechu.
Amesema miongoni mwa sheria hizo, ni kuanzisha Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma (PIA) kwa kubadilisha jina la ofisi ya Msajili kuwa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma (Public Investment Authority- PIA) ili kuakisi majukumu na mwenendo wa ukuaji wa uchumi wa Duniani.
Amesema kuwa kuanzishwa kwa mfuko wa Serikali kwa kufanya uwekezaji wa kimkakati itasaidia kuongeza ufanisi wa uendeshaji, kuokoa mashirika ambayo bila mfuko huo yanaweza kuanguka, pamoja na kuwezesha mashirika ya umma kustahimili ushindani.
“Kuainisha vyanzo vya fedha za mfuko wa uwekezaji wa umma ambapo vyanzo vya fedha za mfuko vitakuwa ni pamoja na sehemu ya maduhuli yatakayokusanya na mamlaka ambayo kiwango chake kitabainishwa kwenye kanuni” amesema. Mchechu.
“Lengo ni kuhakikisha mashirika ya umma yanafanya kazi kwa ufanisi na kuleta faida kwa serikali katika kuhakikisha yanasonga mbele” amesema Mchechu.
Amesema kuwa kwa utaratibu wa kuishirikisha Mamlaka kwenye mchakato wa kuwapata wenyeviti, wajumbe wa Bodi na watendaji wakuu wa taasisi itasaidia katika ufanisi wa kazi.
Mchechu ameeleza kuwa taasisi za umma zinapaswa kuwekewa mifumo rafiki ambayo itasaidia kutengeneza mapato na kuleta tija kwa Taifa.
Katika hatua nyengine amesema kuwa Serikali imefanya uwekezaji wa shilingi trillioni 73 katika Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala wa Serikali 298 ambazo zinafanya shughuli mbalimbali, huku asilimia 86 za taasisi hizo zikitoa huduma za kijamii..
Amesema kuwa kutokana na uwekezaji huo kwa mwaka wa fedha 2022/23 mashirika 108 yameweza kupata mapato ya shilingi bilioni 777.
Mchechu amesema kuwa kwa mwaka 2021/2022 mashirika 136 yameweza kupata mapato ya shilingi Bilioni 645 na mwaka 2020/2021 mashirika 200 yamepata Bilioni 477, huku mwaka 2019/2020 mashirika 236 yameingiza mapato ya Bilioni 696.