Na: Saidina Msangi, WFM, Dodoma.
Wananchi wametakiwa kushiriki kikamilifu katika zoezi la majaribio ya sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Septemba 11, 2021 katika mikoa 13 Tanzania Bara na mikoa mitano Zanzibar, ikiwa ni maandalizi ya zoezi la Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti, 2022.
Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamisaa wa Sensa Tanzania Bara na Zanzibar jijini Dodoma.
Alisema kuwa zoezi la sensa ya watu na makazi ni muhimu kuwezesha upatikanaji wa takwimu zenye uhalisia ili kufanikisha mipango ya maendeleo na ugawaji wa rasilimali za nchi kwa kuzingatia uhitaji.
“Wananchi wajiandae kikamilifu kwa zoezi la majaribio ya sensa ya watu na makazi na wasiruhusu upotoshaji wowote wa zoezi hilo muhimu kwa maendeleo yao binafsi na nchi kwa ujumla,”alisisitiza Dkt. Nchemba.
Dkt. Nchemba aliiagiza Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bara na Visiwani kuhakikisha inatoa elimu kwa umma kwa kuzingatia makundi yao ili kujenga uelewa wa pamoja ikiwa yakiwemo makundi ya wafugaji, wakulima na wavuvi ili wapate ufahamu wa faida ya zoezi la sensa katika sekta zao.
Aliielekeza NBS kuhakikisha rasilimali zitakazohitajika kufanikisha zoezi la sensa ya watu na makazi zinapatikana kwa wakati na kuwashirikisha wadau wanaoweza kusaidia katika upatikanaji wa rasilimali hizo mapema ili zoezi la sensa liwe na mafanikio.
Kwa upande wake Kamisaa wa Sensa Tanzania Bara, Mhe. Anne Makinda, ameishukuru Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushiriki kikamilifu kufanikisha zoezi hilo muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Naye Kamisaa wa Sensa Zanzibar Balozi Mohamed Haji Hamza, alisema kuwa maandalizi ya sensa ya watu na makazi ya majaribio yamekamilika ambapo kwa upande wa Zanzibar mikoa mitano imeteuliwa kwa ajili ya zoezi hilo na upande wa Bara mikoa 13.
“Natoa wito kwa wananchi na viongozi wote kuhakikisha sensa ya watu na makazi ya majaribio inafanikiwa katika maeneo maalumu yaliyotengwa,” alisema Balozi Hamza.
Alisisitiza kuwa sensa ya majaribio ni muhimu ili kuweza kupima madodoso, uwezo, nguvu kazi pamoja na rasilimali zitakazohitajika ili kufanikisha sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.
Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali Tanzania Bara, Dkt. Albina Chuwa na Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar, Bi. Mayasa Mahfoudh Mwinyi, wameishukuru Wizara ya Fedha na Mipango kwa kutoa Sh. bilioni 9.6 kwa ajili ya maandalizi ya sensa h ya wat una makazi. zimetolewa kufanikisha zoezi la sensa ya sita inayotarajiwa kutoa majibu yatakayosaidia Serikali katika upangaji wa mipango ya maendeleo.