NA: FARIDA MANGUBE, MOROGORO.
Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano ya Korea Kusini na Serikali za Afrika kupitia Mpango wa Afrika wa Sayansi, Uhadinsi na Teknolojia PASET umeandaa mkakati wa kuwawawezesha waafrika kukabiliana na changamoto mbalimbali zikiwemo za Magonjwa yasiombukiza na mlipuko, lengo ni kulifanya Bara la Afrika kuweza kutatua changamoto zake lenyewe.
Mpango huo umeanza mwaka 2018 na utadumu kwa zaidi ya miaka 10 unalenga kufadhili masomo ngazi ya uzamivu (PHD) kwa wananfunzi elfu kumi ambapo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ( SUA) ni moja kati ya vyuo vikuu vya mwanzo kushiriki katika mpango huo kati ya vyuo vikuu 15 barani Afrika.
Mratibu wa Mpango wa Afrika wa Sayansi, Uhadinsi na Teknolojia PASET kutoka SUA Prof. Gerald Misinzo amesema mpaka sasa SUA imepokea wananfunzi 43 kutoka Nchi mbalimbali za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania, Kenya, Rwanda, Malawi, Msumbiji, Chadi, Benin, Sudan ya Kusini na Nigeria.
Amesema Wanafunzi hao, watasoma Teknolojia, Sayansi pamoja na Uhadinsi, lengo ni kutatua changamoto za milenia ili kufikia malengo ya Afrika kufikia 2023 ya kila Mwafrika kuwa na Afya bora, kupunguza umasikini na kuwa na uhakika wa chakula.
“Wanafunzi Hawa watasoma Nyanja mbalimbali ikiwemo mazingira Kilimo, utengenezaji wa chanjo dhidi ya magonjwa yanayoathili mifugo, pia kuboresha afya za Binaadam.” Alisema Prof. Misinzo.
Kupitia mpango huo Tanzania itanufaika kwa kupata wataalumu waliobobea katika tafiti za uchambuzi wa vinasaba na kulisaidia Taifa katika kukabiliana na kusambaa kwa magonjwa ya mlipuko, magonjwa yasiyoambukiza pamoja na majanga mengine.
Baadhi ya wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha SUA ambao wamepata ufadhili wa mradi wa PASET, wanasema mpango huo utasaidia Nchi za Afrika kujikwamua kiuchumi kwani zitakuwa na uwezo wa kutatua changamoto zake zenyewe bila ya kutegemea wataalamu kutoka Bara la Ulaya, Asia na Amerika.
Wanasema kwa sasa majanga mengi yanayoikumba Afrika, yakiwemo magonjwa ya mlipuko na kupelekea Mataifa haya kutegemea msaada kutoka nje ya Afrika jambo ambalo halina afya katika masuala ya kiusalama.
Mpango huo utadumu kwa zaidi ya miaka 10 ambapo unasimamiwa na Serikali za kiafrika, tayari Nchi zaidi ya 9 zimejiunga na mpango huo, katika mwaka wa pili na watatu wa masoma wananfunzi watapata fursa ya kutembelea taasisi zilizopo Bara la Asia, Amerika na Ulaya, lengo ni kulifanya Bara la Afrika kuweza kutatua changamoto zake lenyewe.