Maadhimisho ya siku ya wazee Duniani yanayofanyia kila mwaka October 1 mwaka huu wa 2021 yanatarajiwa kuadhimishwa ngazi za mikoa ambapo lengo la maadhimisho hayo ni kuongeza uelewa kwa jamii juu ya masuala ya wazee ikiwemo fursa na changamoto zinazowakabili na namna ya kuzitatua.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kutumwa kwa vyombo vya habari na waziri wa wizara ya Afya maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Dkt Dorothy Ngwajima imeeleza kuwa tayari maelekezo yameshatolewa kwa mikoa yote kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI ambapo kauli mbiu kwa mwaka huu ni“MATUMIZI SAHII YA KIDIGITALI KWA USTAWI WA RIKA ZOTE”.
Dkt Ngwajima alisema kuwa ujumbe huo umewekwa mahususi ili kusisitiza umuhimu wa kutoa nafasi kwa wazee kushiriki katika matumizi ya kidigitali na kuweza kutatua changamoto mbalimbali kwa kufanya shughuli za ubunifu zitakazo waletea maendeleo.
“Kutokakana na kuwa nchi yetu ipo katika uchumi wa kati, matumizi ya kidigitali katika sekta zote za jamii yameongezeka na kutoa matumaini makubwa ya kuharakisha maendeleo ya nchi yetu na kuleta maendeleo endelevu na taarifa ya umoja wa mataifa inaonesha kuwa wanawake na wazee ndio makundi ambayo yameachwa katika matumizi ya kidigitali,”Alisema Dkt Ngwajima.
“Makundi haya hayanufaiki na fursa zinatokana na teknolojia hivyo kama nchi tunawajibu wa kuhakikisha wazee wanapata fursa sawa ya matumizi ya kidigitali ili waweze kunufaika na kukuza ustawi wao,”Alisema.
Alifafanua kuwa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 ilionyesha kuwa Tanzania inakadiriwa kuwa na wazee zaidi ya milioni 1.5 huku wanawake wakiwa, zaidi milioni 1.3 na wanaume wakiwa ni milioni 1.2 sawa na asilimia 5.6 ya wananchi wote ambapo ripoti ya makadirio ya watu ya taifa ya mwaka 2013- 2035 inaonesha makadirio ya ongezeko la wazee na kufikia zaidi ya milioni 2.5 na ongezeko hilo ni kiashiria cha kuendelea kuimarika kwa hali ya upatikanaji wa huduma za msingi kwa kijamii ikiwemo Afya.
“Pamoja na kuimarika kwa huduma za Afya pia tunatakiwa kuimarisha upatikana wa chakula na huduma za matibabu, uboreshaji wa huduma za ulinzi na usalama kwa wazee kwani hayo yote yatachangia kuongezeka kwa umri wa kuishi ambapo serikali imeshachukua hatua mbalimbali za kuboresha maisha ya wazee hapa nchini, Alisema.
Pia alisema kuwa katika kutimiza azma ya kuimarisha huduma kwa wazee serikali ipo katika hatua za mwisho ya mapitio ya sera ya taifa ya wazee ya mwaka 2003 ambapo masula mbalimbali ikiwemo huduma za Afya, mafunzo ulinzi na usalama, hifadhi ya jamii, maandalizi ya wananchi kuelekea uzee na msaada wa kisaikolojia yamewekewa mikakati madhubuti ili kuhakikisha wazee wanapata huduma jumuishi na stahiki kwaajili ya ustawi na maendeleo yao.
Hata hivyo maadhimisho hayo yataambatana na huduma mbalimbali za wazee ikiwemo kupimwa maradhi mbalimbali Kama vile Presha, Kisukari na Tezi dume, msaada wa kisaikolojia na elimu ya kujikinga na UVIKO 19 na kuhamasisha wazee na wananchi kupata chanjo.