*Aonya wanaume wanaowakatisha masomo wanafunzi wa kike
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Ndolage na kuhimiza kiwe kimekamilika ifikapo Novemba 2023 kama walivyoahidi.
“Nimekagua ujenzi wa majengo mapya, naona kazi ni nzuri. Hawa mafundi waendelee na kasi hii na ujenzi ukamilike ifikapo Novemba kama mlivyoahidi ili Desemba, 2023 tuanze usajili wa wanafunzi na Januari, mwakani vijana wetu waanze masomo,” amesema.
Ametoa wito huo leo (Jumapili, Septemba 24, 2023) mara bada ya kukagua uboreshaji wa majengo ya chuo hicho, wakati akizungumza na wananchi waliojitokeza kumpokea katika kijiji cha Bushagara, kata ya Kamachumu, wilayani Muleba, mkoani Kagera.
Amesema katika kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema tuimarishe vyuo vya ufundi stadi nchini ili vijana waweze kupata stadi na kujiajiri. “Chuo hiki kinaweza kuchukua vijana wa ngazi zote hata wa chuo kikuu, hapa wakija wanakuja kupata ujuzi iwe ni wa kuchomelea nondo au kusuka kwani mtu anaweza kuwa na digrii yake lakini hawezi kuchomelea nondo,” amesema.
Amesema Halmashauri nchini zitenge bajeti za kuwasaidia vijana wanaohitimu ili wapate mitaji ya kuanzia kulingana na stadi walizojifunza.
Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA nchini, Bw. Anthony Kasore alisema Serikali ilitoa sh. millioni 903.5 kwa ajili ya upanuzi wa chuo hicho kwa kuongeza miundombinu ya majengo ili kufikia viwango vya chuo cha wilaya.
“Upanuzi wa chuo unahusisha ujenzi wa mabweni mawili yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80; moja la wavulana na jingine la wasichana; bwalo la chakula lenye uwezo wa kuhudumia watu 200; karakana ya umeme; karakana ya uungaji na uundaji vyuma; nyumba ya Mkuu wa Chuo na jiko.”
Alisema mradi huo ulianza kutekelezwa Juni, 2023 na sasa umefikia asilimia 50 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba, 2023. “Upanuzi wa chuo hiki utawezesha kuanza kudahili wanafunzi wa bweni, kwani hivi sasa chuo kinatoa mafunzo kwa wanafunzi wa kutwa pekee, kwa kuwa hakina miundombinu muhimu kama mabweni, bwalo, jiko na nyumba za watumishi.”
Akiwa njiani kuelekea Nshamba, Waziri Mkuu alisimama Kamachumu na kuzungumza na wananchi waliokuwa wakimsubiri njiani. Aliwaeleza miradi inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita na mipango iliyopo ya kuwafikishia huduma katika maeneo yao.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaonya vijana na wanaume wanaokatisha masomo ya wanafunzi wa kike kwa kuwadanganya na lifti za bodaboda.
“Hapa Kamachumu iko changamoto ya wanafunzi wa kike, ndoto zao zinafifishwa. Niwatangazie wanaume: Achana kabisa na matamanio ya mtoto wa kike. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewekeza kwa kumlinda mtoto wa kike, na hii haimaanishi kwamba hamlindi mtoto wa kiume,” alifafanua.
“Rais wetu ametoa fedha nyingi za kujenga shule za sekondari, kwa hiyo Halmashauri tengeni fedha za mapato ya ndani na kujenga mabweni kwani mnao uwezo huo; makusanyo yenu yako juu. Mnakusanya shilingi bilioni saba kwa mwaka, kwa hiyo mkitenga kila miezi mitatu, mtaweza kujenga haya mabweni,” alisisitiza.
Alisema kwa mujibu wa sheria za nchi, mtu akikutwa na kosa la kumpa ujauzito mwanafunzi anastahili kifungo cha miaka 30. “Mwache mtoto wa kike asome kuanzia chekechea hadi chuo kikuu. Mtoto wa mwenzio ni wa kwako, ni mwanao. Siyo mkubwa mkubwa mwenzako,” alisema.
Akiwa njiani kuelekea Magalini kukagua soko la kimataifa la dagaa, Waziri Mkuu aliwasalimia wakazi wa Nshamba na kuwaelezea mpango wa Serikali kusogeza huduma za kijamii kwenye sekta zote.
Waziri Mkuu yuko mkoani Kagera kwa ziara ya siku tatu na leo anazuru wilaya ya Muleba.
(mwisho)
IMETOLEWA NA :
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, SEPTEMBA 24, 2023.