Serikali ya Tanzania imetaka kuwepo na uhuru wa kisera kwa nchi zinazoendelea na maskini ili kujihami na athari za uingizwaji uliokithiri wa bidhaa za kilimo hususan kutoka nchi zilizoendelea.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Prof.Kitila Mkumbo amesema hayo Septemba 16, 2021, katika Mkutano wa Mawaziri wa Kundi la Nchi 33 (G33) wa wanachama wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) uliofanyika kwa njia ya mtandao ambapo aliongoza ujumbe kutoka Tanzania.
Kundi hilo linajumuisha nchi wanachama zenye maslahi yanayofanana ya kutaka uwazi na manufaa katika majadiliano ya WTO yanayohusu Kilimo ambapo lengo la mkutano ni kujadili na kuweka msimamo wa pamoja katika maeneo ya kipaumbele kwenye kilimo.
Katika mchango wake, Mhe. Prof. Mkumbo amebainisha msimamo wa Tanzania kwenye maeneo mbalimbali ambao unaungwa mkono na nchi nyingine wanachama kwenye eneo la misaada ya upendeleo (Domestic Support).
“Msimamo wa Tanzania ni kuwa na makubaliano ya WTO yanayokataza na kuweka vikwazo kwa nchi zilizoendelea wanachama wa Shirika hilo kutoa misaada kwa wazalishaji wao inayoathiri biashara za nchi nyingine wanachama. Hii ni pamoja na kutaka uwepo uwazi kwa nchi ziluzoendelea kwa mfano katika utoaji ruzuku kwa wakulima wao,”amesema.
Pia, amesema Tanzania imesisitiza kutaka nchi zinazoendelea na maskini (Developing and Least Developing Countries-LDCs) wanachama wa WTO kuwa na uhuru wa kuhifadhi chakula kwa madhumuni ya usalama wa chakula.
Mkutano huo umeongozwa na Mwenyekiti Mhe. Muammad Lutfi, Waziri wa Indonesia anayesimamia biashara ambapo ulihudhuriwa pia na Mkurugenzi Mtendaji wa WTO Ngozi Okonjo-Iweala na ulikuwa sehemu ya maandalizi ya nchi hizo katika Mkutano wa 12 wa ngazi ya juu wa maamuzi wa WTO (MC12) unaotarajiwa kufanyika mjini Geneva, Uswisi mwezi Desemba 2021.