Na: Heri Shaaban Ilala
MBUNGE wa Jimbo la Ukonga Jerry Silaa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza miradi ya maendeleo jimboni .
Mbunge Jerry Silaa alitoa pongezi hizo kwa Rais akiwa katika ziara yake Kata ya Kipunguni Wilayani Ilala kwenye mkutano wa hadhara.
“Nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassani katika Jimbo letu ametuletea miradi mikubwa ya Maendeleo ikiwemo kituo cha Afya Kipunguni kilichofunguliwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2022” alisema Silaa.
Mbunge Jerry Silaa alisema katika Jimbo hilo la Ukonga pia wanamshukuru Rais katika utekelezaji wake wa Ilani miradi mbalimbali imetekelezwa kipindi cha Bajeti 2021/2022 kata ya Kipunguni.
Alisema Kata ya Kipunguni Mtaa wa Amani na Machimbo Kivuko cha Wananchi kitajengwa Ili kuwaondolea adha Wananchi wake wakati wa mvua zinaponyesha mawasiliano yanakatika.
Aidha Mbunge Jerry alisema pia katika kata ya Kipunguni miradi mingine iliyotekelezwa madarasa mawili na matundu Kumi ya vyoo shule ya msingi Kipunguni ujenzi umefikia hatua za kupaua na Sekondari ya Kata madarasa 18 na matundu 15 ya vyoo shule hiyo kwa Sasa imesajiliwa pamoja na madarasa NANE ya Uviko .
Akizungumzia Kituo cha Afya Kipunguni kilichofunguliwa na kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru alisema jengo la OPD limekamilika pamoja na mahabara na Sasa Serikali imeleta fedha zingine kwa ajili ya majengo mawili jengo la Upasuaji na jengo la mama na Mtoto ambapo tumeshapokea milioni 250 ujenzi wakati wowote unaanza.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa wananchi eneo la Moshi Bar, Mh Mbunge aliambatana na Meneja wa Dawasa wilaya ya Ukonga ambapo alieleza mpango wa serikali katika sekta ya maji ,ambapo pia alikuwa akipokea kero na kuzitatua papo kwa papo .
Diwani wa Kata ya Kipunguni Stephen Mushi ,alimpongeza Mbunge wa Ukonga Jerry Silaa katika utekelezaji wa Ilani jimboni humo kwa kufanya mambo makubwa katika uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ni makubwa.
Diwani Mushi alisema mikakati mingine ambayo inafanywa na Serikali Kata ya Kipunguni tayari wamepokea shilingi milioni 240 ujenzi wa Sekondari ya ghorofa na pesa za soko la kisasa miradi yote ikikamlika Kipunguni itakuwa ya kisasa fursa mbalimbali zitakuwepo.
Mwisho.