Katibu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi akizungumza wakati wa Kilele cha maadhimisho ya Siku ya afya na Lishe kwa ngazi ya kijiji ambapo iliadhimishwa katika kijiji cha Mpandapanda Kata ya Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya.
Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye Masuala ya Lishe Bi. Afshan Khan akiangalia moja ya nafaka alipotembelea banda la vyakula mchanganyiko wakati wa maonesho ya afua za lishe katika Jiji cha Mpandapanda Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya.
Afisa Lishe Mbeya Jiji Bi. Itika Mlagalila akieleza kuhusu umuhimu wa vyakula vya asili vyenye virutubisho kwa viongozi waliotembelea banda hilo kwa lengo la kuangalia namna utekelezaji wa afua za lishe unavyotekelezwa kuanzia ngazi ya jamii, wakati wa maadhimisho ya siku ya afya na lishe ngazi ya kijiji yaliyofanyika Jijiji cha Mpandapanda Rungwe Mkoani Mbeya.
Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye Masuala ya Lishe Bi. Afshan Khan (wa pili kutoka kulia) akiwa pamoja na wafanyabiashara wa ndizi alipotembelea katika soko la Kiwira Wilaya ya Rungwe mkoa wa Mbeya, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kukagua utekelezaji wa afua za Lishe nchini wakati wa maadhimisho ya siku ya afya na lishe ngazi ya jamii.
Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye Masuala ya Lishe Bi. Afshan Khan, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi pamoja na timu walioyoongozana nayo wakishuhudia zoezi la ugawaji wa chakula wakati wa maadhimisho ya Siku ya afya na Lishe kwa ngazi ya kijiji ambapo iliadhimishwa katika kijiji cha Mpandapanda Kata ya Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya.
Mwanafunzi wa darasa la saba kutoka shule ya msingi ya Goji Rungwe Mbeya Sara Omari akitoa maelezo kuhusu makundi ya vyakula kwa Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye Masuala ya Lishe Bi. Afshan Khan (katikati), Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi wakati wa kukagua mabanda wakati wa siku ya afya na lishe ngazi ya kijiji Wilaya ya Rungwe mkoa wa Mbeya.
Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye Masuala ya Lishe Bi. Afshan Khan akifurahia jambo na mmoja wa watoto walioshiriki katika zoezi la upimaji wa afya wakati wa maadhimisho hayo, kushoto ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi akiteta jambo na mzazi wa mtoto huyo.
Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye Masuala ya Lishe Bi. Afshan (wa kwanza kulia), Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi (katikati) pamoja na timu waliyoongozana nayo wakiwa katika picha ya pamoja na watoto walioshiriki katika maonesho na maadhimisho ya masuala ya afya na lishe ngazi ya kijiji Wilaya ya Rungwe Jijini Mbeya.
Katibu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi pamoja na Mtaalam wa Lishe kutoka UNICEF, Bi. Ruth Nkurlu wakizunguza na mmoja wa wazazi waliojitokeza kupima afya za watoto wao.
Baadhi ya washiriki wa maadhimisho ya siku ya afya na lishe ngazi ya kijiji wakifuatilia mkutano na wanakijiji wa Mpandapanda katika Wilaya ya Rungwe mkoa wa Mbeya.
(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
NA: MWANDISHI WETU
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amewaasa wanaume kuwa mstari wa mbele katika kushiriki masuala ya lishe kwa kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wanawake ili kuwa na taifa lenye lisha bora kuanzia ngazi ya familia.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na wanakijiji wa Mpandapanda katika Kata ya Kiwira Wilaya ya Rungwe mkoa wa Mbeya katika kuadhimisha Siku ya afya na Lishe ngazi ya kijiji ambapo iliadhimishwa kijijini hapo.
Katibu Mkuu Dkt. Yonazi amesema kuwa wanaume wamekuwa mstari wa nyuma katika utekelezaji wa afua za lishe hivyo kukwamisha jitihada zinazofanywa na wakinamama katika kuhakikisha watoto wanapata lishe bora.
“Niwaombe wanaume wote kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha kuwa nchi yetu inakuwa na lishe bora kwa kushirikiana pamoja tutakuwa na watoto wenye afya bora na kuwa na Taifa lenye Lishe bora ili kuchochea maendeleo yetu,” Alisema
Akieleza kuhusu jukumu la ofisi yake amesema, itaendelea kuratibu masuala ya lishe nchini kwa kushirikia na wadau kwa kuzingatia miongozo iliyopo.
“Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuratibu shughuli za Serikali na kuhakikisha miongozo ya masuala ya lishe inatekelezwa ipasavyo ili kila mmoja kujua majukumu yake na kuwa na nia thabiti katika utekelezaji wa masuala ya lishe nchini,” Alisisitiza Dkt. Yonazi
Kwa uapnde wake Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye Masuala ya Lishe Bi. Afshan Khan alipongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuhakikisha Taifa linakuwa na afya bora kwa kuwa na mikakkati inayotekelezeka.
“Tuna ahidi kuendelea kutoa ushirikino wa kila hali kwa kuhakikisha tunaboresha afua za lishe, ninaipongezea Tanzania kwa kuwa na rasilimali zote muhimu, huku nikiupongeza mkoa wa mbeya kwa kuwa na vyakula bora na muhimu kwa afya zetu niwasihii endeleeni kula vyakula vyenye virutubisho kwa kuzingatia mazingira yenu yanaruhusu, yatumieni katika kuimarisha afya kwa kila rika,” alisema Khan .
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mhe. Ben Malisa akitoa salamu za mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo alisema mkoa umeendelea kutekeleza masuala ya lishe kwa kuhakikisha inatatua changamoto za masuala hayo ikiwemo ya udumavu na utapiamlo ambapo alisema ajenda ya lishe imeendelea kupewa kipaumbele mkoani humo.
“Hali ya Lishe kwa watoto wa umri chini ya miaka mitano imeendelea kuimarika kutokana na juhudi kubwa za utoaji wa elimu ya Lishe katika jamii. Kiwango cha watoto wa umri chini ya miezi sita walionyonyeshwa maziwa ya mama pekee kimeongezeka kutoka asilimia 27.3 mwaka 2014 hadi asilimia 71 mwaka 2018,”alisema Ben Malisa
Alibainisha kuwa takwimu zinaonesha kwa mwaka 2022 hali ya Lishe imeimarika ikilinganishwa na mwaka 2018 ambapo kiwango cha udumavu katika Mkoa wa Mbeya kimepungua kutoka asilimia 33.8 hadi 31.5 ingawa kiwango hiki bado kipo juu ya kiwango cha Kitaifa ambacho ni asilimia 30.
Aidha, kiwango cha uzito pungufu kimepungua kutoka asilimia 9.8 hadi 1.4, ukondefu umepungua kutoka asilimia 2.7 hadi 0.6 na uzito uliozidi umepungua kutoka asilimia 5.3 hadi 5.2.
Aliongezea kuwa Juhudi kubwa zimefanyika katika kipindi cha miaka kumi ili kuboresha Afua za Lishe katika Mkoa kupunguza kiwango cha udumavu na aina nyingine zote za utapiamlo. Afua shirikishi za Lishe zinazolenga siku 1000 za mwanzo wa maisha ya mtoto kuhakikisha athari ya muda mrefu katika Lishe, ukuaji na maendeleo ya watoto zinatekelezwa kulingana na Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe wa Sekta Mbalimbali (NMNAP II, 2022-26).