Mbunge wa Jimbo la Segerea Bonah Ladslaus Kamoli akikagua kivuko cha wananchi wa Kata ya Kipawa katika ziara yake ya kutatua kero.
NA: HERI SHAABAN.
MBUNGE wa Jimbo la Segerea CCM Bonah Ladslaus Kamoli amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa shilingi Bilioni 100 kwa ajili ya kutengeneza kingo za mto Msimbazi ajili ya kuzuia mafuriko yasibomoe nyumba zao.
Mbunge Bonah aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika ziara ya kukagua miundombinu ya Kipawa pamoja na kutatua kero za wananchi.
“Wananchi wangu wa bonde la Msimbazi na eneo la Kalakata Serikali inatarajia kujenga kingo katika Bonde la mto Msimbazi ili muondokane na mafuriko mradi huo ukianza kujengwa utaelekeza njia ya mto na kunusuru nyumba zenu za bondeni zisiende na maji ” alisema Bonah.
Katika ziara hiyo Kata ya Kipawa Mbunge Bonah pia alielezea fedha za Serikali shilingi milioni 500 zitakazo tumika kujenga kipande cha Barabara ya Air port kuingilia Kalakata ambapo alisema ujenzi wa kipande hicho cha lami kitaanza baada kujengwa daraja la kivuko cha magari ulipopita mradi wa reli ya kisasa SGR .
Akielezea bomoa bomoa alisema nyumba 46 zitabomolewa kwa ajili ya kupisha mradi huo wa reli ya kisasa ambao umepita kata ya Kipawa.
Amewataka wananchi wa Jimbo hilo wawe wavumilivu barabara nyingi za mitaa ndani ya Jimbo hilo tayari zimeingizwa katika mradi wa DMDP awamu ya tatu na zitajengwa kwa kiwango cha lami.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Kipawa Aidan kwezi alimshukuru Mbunge wa Segerea kuwapatia pesa milioni 13,400,000 za mfuko wa Jimbo ambazo wamezitumia kununua kompyuta mbili kwa kila shule kwa Shule zote tatu za Sekondari zilizo kwenye kata hiyo pamoja na kompyuta mbili kwa ajili ya zahanati ya Kipawa. Kiasi kingine cha fedha wamekitumia kukarabati sehemu ya mapokezi katika zahanati ya Kipawa.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa Reli Saimoni Mbaga alisema mradi wa reli ya Kisasa ni mradi mkubwa sana Kata ya Kipawa ni eneo maalum ambapo kuanzia Pugu Dar es Salaam mpaka Mkoani Morogoro mradi huo umeshaisha kwa asilimia 100 .
Meneja Mbaga alisema kipande kilichobaki ni njia panda Segerea ,Vingunguti na Uwanja ndege kuweka vivuko kukamilisha mradi huo
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Mogo George Mtambalike amewashauri SGR kuweka Ramani zao katika maeneo ya hifadhi ya reli ya kisasa ili wavamizi wasivamie maeneo hayo.
Mwisho.