Serikali ya Tanzania inatarajia kupokea Shehena ya pili ya chanjo ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO 19) aina ya Sinopharm itakayowasili nchini Oktoba 8 mwaka huu, na kufanya idadi ya chanjo hiyo kuongezeka na kufikia 1, 065,00 ambapo shehena ya kwanza ya chanjo kama hiyo ilipokelewa Oktoba 4 mwaka huu.
Ujio wa chanjo hiyo unatokana na mwitikio mkubwa wa watanzania kupata chanjo ya awali iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Julai 28 mwaka huu, ambayo takwimu za Wizara ya Afya zinaonesha kuwa idadi imepanda mara kumi zaidi ya ilivyotarajiwa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam kuhusu taarifa ya maendeleo ya chanjo nchini, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Doroth Gwajima, amesema mafanikio ya chanjo hiyo yanatokana na elimu iliyotolewa kwa jamii kuhusu kujikinga na ugonjwa huo.
“Serikali kupitia kamati zilizoundwa kushirikiana na wadau mbalimbali, inaendelea kutoa chanjo na elimu ya kujikinga na UVIKO 19, tangu Rais Samia Suluhu Hassan azindue chanjo hizo jumla ya watanzania 681,736 wamepatiwa chanjo sawa na asilimia 66 ya dozi zilizosambazwa, kutokana na mwitiko huu baadhi ya mikoa imemaliza chanjo hizo na wanaziomba kwenye mikoa ya jirani, kwa hiyo Serikali imewasikia na sasa zinakuja” amesema Dkt Gwajima.
Aidha, amewataka watanzania kuendelea kujikinga na ugonjwa huo, kwa kufuata kanuni za afya ikiwepo ya kunawa mikono, kutumia vitakasa mikono pamoja na kuvaa barakoa ili kupunguza maambukizi.
“Nawaomba wananchi waendelee kujikinga kama inavyoelekezwa na wataalamu wa afya, ikumbukwe kuwa Oktoba 4 mwaka huu Serikali ilipokea shehena ya kwanza ya chanjo ya UVIKO 19 aina ya Sinopharm, na Oktoba 8 itapokea shehena ya pili ya chanjo hiyo hiyo na kufanya jumla ya chanjo zote kuwa ni milioni moja na elfu sitini na tano (1,065,000), taratibu za uhakiki zinaendelea na tutazisambaza kama ilivyokuwa kwenye chanjo ya Johnson” amesema Dkt. Gwajima.
UVIKO 19 ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na virusi vya Corona ambao ulianzia nchini China mwezi Disemba mwaka 2019, na nchini Tanzania mgonjwa wa kwanza wa ugonjwa huo aliripotiwa Machi 15, 2020