Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt . Pindi Chana ametoa wito kwa wadau wa utalii wa ndani na nje ya nchi hususan Wakala wa Biashara za Utalii, watoa huduma za malazi, Wakala wa Safari na waongoza watalii kuchangamkia fursa za kiuchumi na kijamii zitakazotokana na Onesho la Kimataifa la Utalii la Swahili International Tourism Expo (S!TE) litakalofanyika jijini Dar es salaam kuanzia tarehe 21 hadi 23, Oktoba, 2022.
Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ametoa wito huo Jijini Arusha alipokua akizungumza na waandishi wa habari kuhusu onesho hilo kubwa la Utalii ambalo ni la Sita litakalofanyika katika wa mikutano wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam Tanzania.
Waziri Pindi Chana amezitaja fursa hizo kuwa ni pamoja na kutangaza biashara, kutengeneza mtandao wa biashara na kutoa huduma mbalimbali wakati wa onesho hilo.
“Ni matarajio ya Serikali kuwa taasisi na makampuni mbalimbali yatajitokeza kwa wingi katika kufadhili shughuli mbalimbali ili kunufaika na fursa za kujitangaza kupitia onesho hili la S!TE” Aliongeza Mhe. Balozi Dkt. Chana.