MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amewataka wananchi kutambua thamani ya Mwenge wa Uhuru na kushiriki shughuli ambazo umekuwa ukihamasisha.
Waziri Mhagama ameyasema hayo wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa, Kilele cha Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2021 na kumbukizi ya miaka 22 ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere katika Viwanja vya Mazaina Wilaya ya Chato mkoani Geita.
Waziri alieleza kuwa, shughuli za Mbio za Mwenge wa Uhuru zinazotarajiwa kufanyika tarehe 14 Oktoba, 2021 katika Uwanja wa Magufuli Wilayani humo huku zikiwa zimebeba kaulimbi isemayo; “TEHAMA ni Msingi wa Taifa Endelevu; Itumie kwa Usahihi na Uwajibikaji”
Waziri Mhagama alisema, Mwenge wa Uhuru na Mbio zake umeendelea kuwa muhimu kwa taifa hadi leo kwa kujenga undugu, umoja, mshikamano na kudumisha amani pote unapopita bila kujali itikadi za kisiasa, dini wala makabila yetu.
“Umuhimu huu unatokana na ukweli kwamba, misingi hii tunahitaji leo na kesho kujenga kuliko wakati wowote ule ili tuweze kujenga taifa lisilokuwa na dhuluma, unyonge, rushwa, ubaguzi, ukabila, udini wala vitendo vya kifisadi”alisisitiza.
Aidha aliongezea kuwa Mbio hizo zimeendelea kuhamasisha wananchi kwa kushirikiana na Serikali yao katika kubuni na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika nyanja za kilimo, ufugaji, uvuvi endelevu, uboreshaji na ujenzi wa miundombinu ya barabara, afya, elimu, maji, umeme na huduma za kijamii katika maeneo yote nchini.
“Kwa mfano, katika kipindi cha mwaka 2010-2019, jumla ya miradi 14,145 yenye thamani ya Shilingi za Kitanzania Trilioni 8.03 ilihamasishwa, iliwekewa mawe ya msingi, na kuzinduliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru,”alieleza.
Aliongezea kuwa, kwa miradi ambayo imebainika kuwa na mapungufu Serikali imekuwa ikichukuliwa hatua katika sekta mbalimbali ili kuendeleza jitihada za kujiletea maendeleo.
Akieleza sababu za Mbio hizo kuwa Maalum na kuhitimishwa Wilayani Chato alisema kwa mwaka huu ni sehemu ya historia muhimu kwa nchi yetu kwa kuendelea kuenzi mchango wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kuendelea kutambua na kuenzi kwa matendo.
“Sote tunafahamu kuwa, Mwenge wa Uhuru mwaka huu unakimbizwa wakati Watanzania tukikumbuka kuondokewa na Kiongozi wetu mpendwa Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli aliyefariki akiwa madarakani, ndio maana kilele cha Mbio hizi kinafanyika Chato alikozaliwa ili kumuenzi,”alisema waziri Mhagama.
Aidha Mbio za Mwenge mwaka huu zinafanyika wakati Tanzania imeweka Historia mpya tangu Uhuru ya kuongozwa na Rais Mwanamke Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndio maana Mbio hizi zilizinduliwa Mkoani Kusini Unguja-Zanzibar alikozaliwa.
Alieleza mbio hizi zimekimbizwa katika Mikoa 31 na Wilaya za Kiutawala 150 tu badala ya kukimbizwa kwenye Halmashauri za Wilaya 195 kama ilivyozoeleka. Vilevile, Vijana sita wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa wameteuliwa kutoka kwenye Jeshi letu la Wananchi Tanzania tu.
Kwa upande wake Mkoa wa Geita Mhe. Rosemary Senyamule aliwaasa Wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo na kuhakikisha wanaunga mkono jitihada za serikali huku wakiitumia wiki hii kama fursa katika mkoa.
Alisema mkoa umejipanga kuendelea kupokea viongozi mbalimbali watakao fika kwa ajili ya shughuli hiyo huku alieleza mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
“Tunashukuru mkoa kupata heshima hii, na niwaombe wananchi mjitokeze kwa wingi kujumuika katika kuifanikisha siku hii maalum huku mkiendeleza amani, umoja na mshikamano wenu”alisema Rosemary.