Rogatus Mativila Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) akiongozana na Mhandisi Motta Kyando Meneja wa TANROADS mkoa wa Kilimanjaro wakimsikiliza Mhandisi Mhandisi Charles Lubazibwa ambaye ni mkaguzi wa barabara wakati akitoa maelezo kuhusu ukamilishaji wa maandalizi ya jiwe la ufunguzi wa barabara hiyo.
Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kufungua kipande cha barabara ya SanyaJuu-Elerai iliopo wilaya ya Siha, Kilimanjaro chenye urefu wa kilometa 32.2
Kipande hicho ni sehemu ya ujenzi na ukarabati wa barabara kubwa yenye urefu wa kilometa 98.2 unaotekelezwa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ambacho ni kutoka Bomang’ombe – SanyaJuu-Kamwanga.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Nchini (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila amesema ufunguzi wa barabara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi mwaka CCM 2020/25.
Eng; Mativila amesema TANROADS imedhamiria kuhakikisha inasimamia kwa ukamilifu ujenzi wa madaraja na barabara mbalimbali nchini ili kuhakikisha inatimiza ndoto ya Serikali kuwa na miundombinu bora ya barabara na madaraja.
“TANROADS imedhamiria kumaliza barabara zote kwa wakati hasa zile za kimkakati ili kutimiza azma ya serikali katika kuharakisha maendeleo na kufungua mikoa kwa mikoa na nchi zingine’’ amesema Eng. Mativila.
Amesema Serikali imekuwa ikitoa fedha za ujenzi wa barabara nchini lengo kubwa la TANROADS ni kuhakikisha barabara hizo zinakuwa bora na kudumu kwa muda mrefu zaidi.
‘’Barabara zinazojengwa sehemu mbalimbali pamoja na hii inayotarajiwa kuzinduliwa na Mheshimiwa Rais Samia Imesanifiwa kudumu kwa miaka 20 , hivyo wananchi wana wajibu mkubwa wa kuitunza na kuilinda’’ alisema Eng. Mativila.
Kwa upande wake, Mhandisi Mradi wa barabara hiyo, Eng. Miraji Hassan alisema barabara itakafunguliwa na Rais Samia ni kipande cha kilometa 32.2 ambacho kimejengwa kwa gharama ya sh. Bilioni 60
Eng. Hassan alisema mradi mzima wa barabara hiyo ni kilometa 98.2 na uligawanya kwa awamu tatu, ambapo awamu ya kwanza ilikuwa Bomang’ombe-SanyaJuu ambayo ilikuwa kilometa 24, ambapo sehemu kubwa ya barabara hiyo ilifanyiwa ukarabati.
Aidha, alisema sehemu ya pili ilikuwa na ujenzi wa barabara kutoka SanyaJuu – Elerai yenye kilometa 32.2, ambayo inatarajiwa kufunguliwa na Rais Samia huku sehemu ya tatu ni kutoka Elerai-Kamwanga, ambapo usanifu wa barabara hiyo uko tayari kutoka Tanzania hadi mpakani Kenya.