WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) ishirikiane na wadau wa masuala ya utalii ukiwemo uongozi wa kambi ya kupokea watalii ya Asilia kuitangaza hifadhi ya kisiwa cha Rubondo.
Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Oktoba 15, 2021) wakati akizungumza na baadhi ya watumishi wa TANAPA pamoja na wa kambi ya Asilia Rubondo akiwa katika ziara fupi ya kuhamasisha utalii katika hifadhi ya Kisiwa Rubondo, Geita.
Amesema ili sekta hiyo iweze kupata tija uongozi wa TANAPA unapaswa kuwa karibu na wadau wa masuala ya utalii. “Endeleeni kuwasikiliza na kushirikiana nao katika kutatua changamoto zinazowakabili ili kuongeza idadi ya watalii.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ameupongeza uongozi wa kampuni ya Asilia kwa uwekezaji wake katika sekta ya utalii nchini na ameusisitiza uendelee kupanua wigo ili kukuza sekta hiyo na kuongeza tija.
Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA Kanda ya Magharibi, Martine Loibooki amemshukuru Waziri Mkuu kwa hatua yake ya kuhamasisha utalii katika hifadhi ya Rubondo na kwamba watayafanyia kazi maelekezo yote aliyoyatoa.
Hifadhi ya Kisiwa cha Rubondo ina ukubwa wa kilometa za mraba 457, iko kaskazini magharibi mwa Tanzania ndani ya ziwa Victoria ziwa ambalo ni la pili kwa ukubwa duniani. Hifadhi hiyo inaundwa na visiwa vidogo 11 kikiwemo na kisiwa cha ndege.
Kisiwa cha Rubondo ndilo eneo pekee katika ziwa victoria lenye mazalia ya samaki yaliyohifadhiwa kisheria. Samaki wanaopatikana katika kisiwa hicho ni pamoja na sato na sangara ambao wanaweza kukua hadi kufikia uzito wa hadi kilo 100.
Fukwe za kisiwa hiki ni miongoni mwa makazi ya pongo na nzohe. Aidha hifadhi hii ni maskani makuu ya mamba, ndege na samaki kama zumbuli, chechele na taisamaki, mbali na ndege hao kisiwa hiki ni makazi ya aina nyingine nyingi ya ndege wa majini na mimea kadhaa ambayo hutoa harufu nzuri ya kuvutia.
Wanyama wakazi wa hifadhi ya Rubondo ni pamoja na viboko, pongo, nzohe, fisi maji, mamba na pimbi wanashirikiana makazi na wanyama waliohamishiwa katika hifadhi hiyo kama sokwe, tembo, mbega weusi na weupe na twiga.
Pia, aina nyingine ya utalii inayofanyika katika hifadhi hiyo ni pamoja na uvuvi wa samaki wa kitalii.(sport fishing).