Home LOCAL JUKWAA LA WAHARIRI TANZANIA TEF YALAANI KUSHABULIWA KWA WAANDISHI WA HABARI NGORONGORO

JUKWAA LA WAHARIRI TANZANIA TEF YALAANI KUSHABULIWA KWA WAANDISHI WA HABARI NGORONGORO

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limesikitishwa na tukio lililofanywa na vijana wa Kimasai (Morani) zaidi ya 200 katika Kata ya Enduleni, wilayani Ngorongoro la kuwashambulia waandishi wa habari na kuwatia majeraha makubwa wakiwa kazini.

Agosti 15, 2023, vijana hao wakiwa na silaha za jadi (mapanga, mikuki, sime na mishale), waliwavamia wanahabari wakati wanakusanya taarifa kutoka kwa Wamasai wanaoishi Ngorongoro wanaotaka kuhama kwa hiyari kutoka katika Kijiji cha Enduleni kilichopo ndani
ya Hifadhi ya Ngorongoro, Arusha waende kuishi Msomera wilayani Handeni, Tanga.

Wanahabari waliofikwa na mkasa huo ni Ferdinand Shayo (ITV), Denis Msacky (Media Brain), Habib Mchange (Jamvi la Habari), Elia Kinian (Channel Ten), Janeth Joseph (Mwananchi), Dickson Busagaga (Clouds Media) na mkalimani wao Lengai Ngoishiye. Baada ya wanahabari hao kushambuliwa, walipelekwa kupata matibabu katika Hospitali ya FAME iliyopo Karatu.

Waandishi hao wanamtuhumu Mbunge wa Ngorongoro, Emmanuel Ole Shangai kuwa alimtuma Katibu wake wakati yuko mnadani na Diwani kuwatawanya wananchi wasizungumze na waandishi wa habari. Baada ya kuona wananchi hao hawatii katazo lake, akawaashiria vijana wa Kimasai washambulie waandishi hao wa habari.

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) linakemea vikali tukio hili la kijinai lililolenga kuwaumizi waandishi wa habari waogope kufanya kazi yao ya kuhabarisha wananchi. TEF pia inakemea hatua ya wanasiasa kuhamasisha wananchi kujichukulia sheria mkononi. Imekuwa kawaida baadhi ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGOs) kuwaambia Wamasai kuwa adui yao mkubwa ni vyombo vya habari nchini na sasa kauli hizi zimethibitishwa kwa tukio hili la kijinai. Kazi ya uandishi wa habari hatuifanyi kwa hisani bali ni haki ya Kikatiba inayotolewa chini ya Ibara ya 18 ya Katiba yaTanzania (1977) na Sheria ya Huduma za Habari (MSA 2016) kama ilivyorekebishwa mwaka 2023. Kwa namna yoyote, ile ni kinyume cha Katiba na Sheria za nchi kuwashambulia waandishi wakiwa wanatekeleza majukumu yao.

TEF tunaomba Jeshi la Polisi kuchunguza, kuwasaka na kuwakamata wote waliohusika na shambulio hilo na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria. Tunawaonya wanasiasa wanaotumia shida za wananchi, uelewa mdogo wa wananchi na hila kujitengenezea umaarufu kwa kuwahadaa wananchi kuwa wanawatetea wabaki Ngorongoro, ilihali moyoni wakifahamu

fika kuwa wanahatarisha maisha ya wapigakura wao waendelee kuliwa na wanyama.

Lakini pia, TEF inafatilia kwa karibu mfululizo wa matukio ya kushambuliwa waandishi wa habari, kuwadhalilisha kwa kuwatenga katika makundi ya “waandishi wa kisasa” na “wa zamani”, manyanyaso na matusi kwa waandishi kupitia mitandaoni, ambapo tunawasihi wananchi na viongozi wenye hulka hizo kuziacha mara moja kwani hazina afya kwa maendeleo ya taifa letu. TEF tunasubiri kusikia hatua za kisheria zitakazochukuliwa dhidi ya watu hawa wanaofanya vitendo vya kihuni visivyokubalika katika utawala wa sheria. Ni matarajio yetu, watuhumiwa wote watakamatwa na watachukuliwa hatua za kisheria ili iwe funzo kwa wengine.

Mungu ibariki Tanzania.
JUKWAA LA WAHARIRI TANZANIA (TEF)

 

Previous articleMKURUGENZI TABORA MANISPAA ELIAS MAHWAGO KAYANDABILA AMSHUKURU RAIS SAMIA KUTOA FEDHA ZA UJENZI MIUNDOMBINU YA ELIMU KIDATO CHA TANO
Next articleJK ATETA NA KAMATI YA UTATU YA SIASA,ULINZI NA USALAMA (SADC_TROIKA) MJINI LUANDA_ANGOLA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here