Picha ya pamoja.
MTENDAJI Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila, amewataka wasafirishaji wote nchini kubeba mzigo kwa kiwango kinachohitajika ili ukiongezeka uzito kutokana na mzigo kusogea mbele ama kurudi nyuma ndiyo wafidie asilimia tano zilizowekwa na serikali.
Ametoa ufafanuzi kuwa utaratibu wa asilimia tano ya uzito wanaopewa wasafirishaji katika magari, unalenga kufidia uzito utakaoongezeka kutokana na miinuko na matuta ya barabarani.
“Ikitokea mzigo umecheza, umesogea mbele ama kurudi nyuma kwenye zile Akseli unapopima ukiongezeka asilimia tano unasamehewa,” amebainisha.
Eng. Mativila amesema hayo leo wakati akifungua semina ya kuelimisha wadau wa sekta ya usafirishaji, juu ya sheria ya Afrika Mashariki ya udhibiti wa uzito wa magari ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018.
“Kuna kitu kinaitwa ‘Five Percent Tolerance’ ambacho kilikuwekwa na serikali kwamba katika mzigo utakaochukua utakapokwenda kupima katika mzani, kwa sababu unatembea kwenye barabara na zina matuta sehemu nyingine zina mashimo hata namna ya kuweka mzigo ndiyo maana ilitolewa asilimia tano ya bure kwa wasafirishaji,”. Ameongeza Eng. Mativila.
Ameeleza kuwa changamoto iliyopo ni kwamba wasafirishaji wanajaza mizigo na kufidia asilimia hizo tano, hivyo wanapokwenda katika mizani uzito unaongezeka
Amewataka kutii sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kudhibiti uzito wa magari barabarani, ili kutunza miundombinu hiyo iendelee kutoa huduma inayotarajiwa na serikali.
Aidha amewaasa watumiaji wa barabara kuhakikisha wanazingatia uzito unaokubalika huku akiwataka watendaji wa TANROADS kutoa huduma kwa wakati na kuzingatia uzalendo na uadilifu.
Mtendaji Mkuu huyo, amewasisitiza wadau hao, kuendelea kutunza miundombinu ya barabara ili huduma tarajiwa iendelee kupatikana bila kucheleweshwa.
Amesema shabaha ya mafunzo hayo ni kutoa uelewa wa sheria hiyo na kupitia jukwaa hilo, taasisi yake itapokea changamoto, ushauri, maoni na wataalamu watatoa ufafanuzi pale utakapohitajika.
Amebainisha kuwa anatarajiwa baada ya mafunzo hayo, makosa ya uzidishaji uzito katika barabara yatapungua na hivyo kutakuwa na ushirikiano katika kuzitunza ili zilete tija inayokusudiwa.
“Ninatarajia kuwa baada ya mafunzo haya makosa ya uzidishaji wa uzito katika barabara zetu, yatapungua na hivyo basi tutashirikiana kuzitu za ili zilete tija inayokusudiwa,” amesema Eng Mativila.
Amsema serikali inagharamia fedha nyingi katika ujenzi wa barabara ili wasafirishaji wazitumie kusafirisha mizigo mbalimbali.
“Ni vyema mtambue kwamba hivi vitu ni vyenu, elimu inatolewa ili muelewe kwamba sio suala la kukwepakwepa, ni suala la kutambua kwamba barabara hiyo utakapoipondaponda basi nawe shughuli yako itakufa maana utashindwa kupeleka biashara zako mahali panapotakiwa kupelekwa,” amesema.
Ameongeza kuwa upatikanaji wa huduma bora na nafuu, unategemea uwepo wa miundombinu bora ya usafirishaji hivyo, ni wajibu wao kuilinda.