Na: Mwandishi Wetu, GEITA.
Kampuni ya Puma Tanzania imetoa zawadi kwa washindi wa Shindano la michoro ya alama za Barabarani ikiwa ni Katika mpango wake wa kutoa mafunzo ya elimu ya usalama barabarani kwa lengo la kupunguza ajali zinazotokea mara kwa mara nchini ambapo mpaka sasa mpango huo umeweza kuwafikia wanafunzi 110,000 kutoka katika shule za msingi zaidi ya 100 katika mikoa ya Dar es Salaam , Geita,Ruvuma, Dodoma na Visiwani Zanzibar.
Kampuni hiyo imewawezesha wanafunzi hao kupata mafunzo ya usalama barabarani na kuwashindanisha kuchora michoro inayotoa ujumbe unaolenga kuelezea usalama baarabarani na kisha washindi kujinyakulia fedha ambazo zinatolewa na Kamuni ya Puma ambayo inatoa elimu hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Amend.
Akizungumza Oktoba 20, 2021 wakati wa utoaji wa zawadi kwa wanafunzi walioshinda katika uchoraji wa michoro ya usalama barabarani kutoka Shule tano za msingi mkoani Geita, Ofisa Usalama ba Mazingira wa Kampuni ya Puma Ambokege Minga ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo amesema wanatambua umuhimu wa mafunzo hayo kwa wanafunzi.
Akifafanua zaidi amesema Puma Energy Tanzania Ltd imetoa zawadi kwa wanafunzi wa shule za msingi walioshinda shindano la michororo ya usalama barabarani kwa mwaka 2020-2021 mkoani Geita na kwamba tukio hilo la utoaji zawadi linahitismisha mradi huo kwa kipindi cha mwaka huu uliofanywa Kampuni ya Puma kwa ushirikiano na Shirika lisilo la kiserikali la AMEND.
“Mpango huu kaika Mkoa wa Geita ulihusisha mafunzo kuhusu usalama barabarani katika shule tano na wanafunzi wasiopungua12,000 wamefikiwa pamoja na shindano la uchoraji wa michoro inayo hamasisha usalama barabarani.
Katika utoaji huo uliohudhuriwa pia na maofisa wa ngazi mbalimbali wa Jeshi la Polisi ,Kikosi cha Usalama Barabarani, Mwakilishi huyo wa Kampuni ya Puma amesema wameamua kuja Geita kwa sababu ya ukuaji wa haraka wa mji huo ambapo shughuli za kijamii na ongezeko la watu na magari ambayo yanahatarisha usalama wa watoto wanapokwenda shule na kurudi nyumbani.
“Mpaka sasa tumeweza kufundisha jumla wanafunzi zaidi ya12,000.. wa shule za msingi katika shule 5 (Tano) za mji wa Geita na hii ikiwa ni mara ya pili kuendesha mafunzo haya mkoani Geita.Mafunzo haya ya usalama barabarani na uchoraji ni kipaumbele chetu kwa lengo la kuwapa uelewa watoto hususani wa shule za msingi juu ya namna bora ya matumizi ya barabara.
“Lengo kubwa la mpango huu ni kuwafanya watoto hawa kuwa na uelewa wa matumizi ya barabara wakiwa bado wadogo. Tunaamini kwa kufanya hivyo tunawaongezea uelewa kuhusu dhima nzima ya usalama barabarani kwa waTanzania wengi Zaidi. Mpango huu pia kwa mwaka huu unategemea kufanyika katika mikoa ya Dar es salaam, Dodoma na visiwani Zanzibar.
“Jumla ya shule 20 zimefikiwa kwa mpango huu kwa mwaka 2021. “Lengo letu kama kampuni ni kuongeza wigo ili kufikia shule nyingi Zaidi nchi nzima. Mkurugenzi wakampuni ya Puma kupitia mwakilishi wake ameahidi pia kuwa Puma Energy itaendelea kuwekeza katika kampeni ya usalama barabarani ikishirikiana na serikali kupitia jeshi la Polisi ili kuokoa maisha ya watanzania,”amesema..
Kwa upande wake Mkaguzi Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Geita Emmanuel shagaya amewaomba wanafunzi waliopata mafunzo hayo wameombwa kufikisha ujumbe unaohusu usalama barabarani.
“Watoto mkifika nyumbani waiteni wazazi wote wawili kisha kaeni chini na baada ya hapo waambieni baba na mama wazingatie usalama wao wawapo barabarani pamoja na kuzingatia usalama wa wengine, tukifanya hivyo tutakuwa salama na tutapunguza ajali za barabarani zitapungua na kuokoa Taifa.
Amesisitiza elimu ya mafunzo ya usalama barabarani ni muhimu kwani kuwepo kwa shughuli nyingi za kijamii zimechangia ongezeko la ajali,lakini kupitia elimu hiyo ni matumaini yao zitapungua.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kalangalala wilayani Geita Prudence Temba amesisitiza umuhimu wa jamii kuzingatia matumizi sahihi ya barabarani huku akiwaomba wanafunzi kufikisha elimu hiyo kwa wazazi au walezi.
Pia amesema kuna wanafunzi ambao wamekuwa wakipanda bodaboda,hivyo wasikubali kupanda bodaboda bila kuvaa kofia ngumu, amewasisitiza wanafunzi hao wahakikishie wanapopakiwa katika magari na wazazi wao kama hawajafunga mikanda,basi waambie wavae na kuwakumbusha ulazima wa kufuata sheria za barabarani.
“Katika eneo letu la Kalangalala kuna muingiliano mkubwa wa watu, hivyo tunaomba mtusaidie kupaka rangi katika maeneo ya wavuka kwa miguu, alama zimefutika na kusabababisha kutoonekana vizuri.Pia tunatoa ombi kwa Kampuni ya Puma itusaidie kutejengea ukuta wa shule ya Msingi Kalangalala, matofali yapo, hivyo mtusaidie michanga na mambo mengine, wala hatutaki fedha,”amesema.
Mgeni rasmi kutoka Ofisi ya Ofisa Elimu Mkoa wa Geita amesema Masumbuko Magang’bila amewasukuru Puma kwa kupeleka mafunzo hayo lakini ni vema wakaendelea kutoa elimu hiyo muhimu yenye lengo la kuokoa maisha ya watu.”Tunapotoa mafunzo kwa wanafunzi maana yake tunakwenda kupeleka elimu hiyo ngazi ya chini kabisa, wanafunzi ambao tunawaona shuleni wana wazazi na walezi wao ndio sisi.”
Pia amesema wamefurahishwa na shindano la michoro kutoa elimu ya usalama barabarani na kubwa zaidi zawadi ya Sh.milioni nne ambayo shule itakayotoa mshindi wa kwanza itatoa hamasa kwa shule kuwa mabalozi wazuri, lakini kwa mwanafunzi atakayeshinda na kushika nafasi ya kwanza kwa uchoraji sh.500,000 itakwenda kuongeza hamasa kwa wanafunzi katika kuchora lakini kuwa balozi wa usalama barabarani yeye na wazazi wake.
Mwalimu wa Shule ya Msingi Nguzo Mbili amesema siri ya ushindi wa shindano hilo ni kujamini ,kujituma na kuwapa wanafunzi kutambua namna ya kutumia vipaji vyao na hatimaye wameibuka kidedea na kushinda Sh.Milioni Nne wakati mshindi wa kwanza kutoka shule hiyo ameibuka mshindi kwa kuchukua nafasi ya kwanza na kushinda Sh.500,000.
Mshindi wa kwanza wa mashindano ya kuchora mchoro wa usalama barabarani ni Victoria Michael wa Shule ya Msingi Nguzo mbili,mshindi wa pili ni Zabibu Stanford Shule ya msingi Nyankumbu aliyepata Sh.300,000 na mshindi wa tatu ni Paul Haruna wa shule ya Msingi Nguzo Mbili aliyepata Sh.150,000.