Na: Mwandishi Wetu.
MKUU wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam Jokate Mwegelo, ametoa maelekezo kwa Wakala wa Barabara (TANROADS) na Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA), kuzingatia uwekaji wa alama za usalama barabarani katika maeneo ya shule wakati wa kuandaa michoro ya ujenzi wa barabara hizo na katika utekelezaji wake.
Aliyasema hayo, Dar es Salaam, alipokuwa akizindua alama za usalama barabarani katika Shule za Madenge na Ruvuma wilayani humo, ambazo zimetengenezwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Amend huku akitaka pia jeshi la Polisi wilayani humo, kuhakikisha linasimamia kikamilifu masuala ya usalama barabarani huku akisisitiza pia jamii kufuata sheria hizo.
“Naelekeza TARURA na TANROADS, wakati mkiandaa michoro ya barabara na katika utekelezaji mzingatie kuweka alama hizi katika maeneo muhimu hasa ya shule. Zingatieni hili ili tupunguze ajali hizi zinazosababisha vifo na ulemavu,”amesema.
Kuhusu Jeshi la Polisi Jokate ameisitiza wasimamie kikamilifu sheria za usalama barabarani na kuchukua hatua stahiki kwa watu wanao vunja sheria hizo.
“Serikali yetu inaboresha kwa kiasi kikubwa barabara .Wilaya yetu ya Temeke pia imepata barabara nzuri. Lakini halii imekuwa changamoto. Watu hawazingatii sheria za usalama barabarani. Wanaendesha vyombo vya usafiri kwa kasi bila kujali kuna watumiaji wengine wa barabara,”amsema.
Akiizungumzia Amend, Jokate amewapongeza kwa ujitolea kuweka alama za barabarani katika maeneo ya shule hizo za Madenge na Ruvuma pamoja na kutoa elimu kwa wanafunzi na watumiaji wa barabara.
“Amend kwa kweli mmetusaidia mno Temeke.Mmelinda uhai wa watoto wetu.Mmefanya jambo zito na niwahakikishie serikali itaunga mkono jitihada zenu hizi kwa asilimia miamoja,”alieleza Jokate.
Kwa upande wake Meneja wa Amend hapa nchini, Simon Kalolo, amesema wamekuwa wakijitolea kutoa elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi katika mikoa mbalimbali nchini na kuweka alama hizo ili kuzua ajali.
“Dhamira yetu ni kuona wanafunzi ,wadau wa elimu na jamii yote inakuwa salama dhidi ya ajali za barabarani. Katika shule za Madenge n a Ruvuma, tumejitolea kuandaa michoro ya usalama barabarani, vivuko na kuwapa elimu wanafunzi ili wawe mabalozi wazuri wa usalama barabarani, “amefafanua Kalolo.
Wakati Diwani wa Kata ya Temeke, Omari Babu, ametumia nafasi hiyo kuipongeza Amend kwa msaada wa alama hizo na kueleza kuwa zitasaidia kupunguza ajali za barabarani huku akiitaka jamii kuzingatia sheria.
Mwisho.