Meneja wa fedha na mauzo wa Shirika la Shule Direct Peter Kungu (kulia) akijadiliana jambo na Meneja Mahusiano wa Taasisi hiyo Bi. Narindwa Msongole katika maadhimisho ya Wiki ya Asasi za Kiraia (azaki) yanayofanyika kwa siku sita Jijini Dodoma
Meneja wa fedha na mauzo wa Shirika la Shule Direct Peter Kungu (kulia) akitoa maelezo namna ambavyo Shirika hilo linavyotekeleza majukumu yake kwa wa wadau waliofika kutembelea kwenye Banda lao kujifunza na kufahamu shughuli zao. (wa pili kulia) ni Bi. Narindwa Msongole Meneja Mahusiano wa Taasisi hiyo.
Meneja wa fedha na mauzo wa Shirika la Shule Direct Peter Kungu akitoa ufafanuzi wa jinsi ambavyo Programu yao waliyoisambaza mashuleni inavyofanya kazi.
Na: Hughes Dugilo, DODOMA.
Wito umetolewa kwa watanzania wote nchini kuunga mkono juhudi za Serikali za kuendeleza na kukuza Sekta ya TEHAMA ambayo imekuwa kwa kasi kubwa na kusaidia katika kukuza uchumi wa nchi na maendeleo kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Meneja Mahusiano wa Taasisi ya Shule Direct Bi. Narindwa Msongole katika maadhimisho ya Wiki ya Asasi za Kiraia (azaki) yanayofanyika kwa siku sita Jijini Dodoma ambaye Taasisi yao inayojihusisha na masuala ya TEHAMA, amesema kuwa juhudi za Serikali katika kukuza Sekta hiyo zinapaswa kuuungwa mkono na wadau wote ili kuiwezesha jamii hususani wanafunzi kufikiwa na huduma hiyo kwa lengo la kuanza kuwajengea uwezo wa matumizi ya TEHAMA mapema.
Ameongeza kuwa katika kuhakikisha hilo linafanikiwa, Shirika lao limekuwa na Majukwaa mbalimbali ikiwemo Elimika LMS ambayo inawawezesha wanafunzi wa Shule za Sekondari kupata maudhui ya kujifunzia katika kompyuta za Shule.
“Majukwaa haya ya Shule Direct yamekuwa yakitumiwa kwa takribani miaka saba sasa ambapo katika kipindi chote hicho kumekuwa na matokeo chanya kwa watumiaji hao hususani wanafunzi na walimu wa sekondari na sasa tupo katika mchakato wa kutengeneza maudhuhi kwaajili ya wanafunzi wa shule za msingi” amesema Narindwa.
Kwa upande wake Meneja wa fedha na mauzo wa Shirika hilo Peter Kungu ameeleza namna ambavyo teknolojia hiyo inavyowawezesha wanafunzi kuweza kutatua changamoto mbalimbali katika kujifunza na kufundishia.
“Zipo changamoto nyingi ambazo Majukwaa yetu yameweza kuwasaidia wanafunzi na walimu kuzitatua ambazo ni pamoja na upatikanaji wa maudhuhi ya kujifunza na kufundishia kwa walimu na wanafunzi, na kwa upande wa wazazi tumewawezesha kuwapatia taarifa mbalimbali zinazohusu watoto wao wawapo shuleni na kuwapatia masomo na makala mbalimbali zinazowawezesha kuwasaidia watoto wao majumbani” amesema Peter.
Ameongeza kuwa majukwaa hayo imewasaidia walimu kujiongezea ujuzi na kipato pia.
Maadhimisho ya Wiki ya AZAKI yanaendelea Jijini Dodoma ikiwa ni jukwaa pekee nchini linalowaleta kwa pamoja wadau wakuu wa maendeleo ikiwemo Serikali, Sekta binafsi na Asasi za Kiraia pamoja na wananchi kwa lengo la kujadili masuala yanayohusu ustawi wa nchi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.