Home LOCAL WAZAWA WA MARA WATAKIWA KUWEKEZA KWAO.

WAZAWA WA MARA WATAKIWA KUWEKEZA KWAO.

MKUU wa Wilaya (DC) ya Bunda, Joshua Nassari (aliyevaa suti na shati jeupe), Katibu tawala (DAS) wa wilaya hiyo(Aliyevaa kaunda suti), Mkurugenzi wa Hoteli ya Password, Nelson Shirima(mwenye t.shirt na kofia nyeupe) wakiwaa na madereva wa bodaboda wakati wa uzinduzi wa hoteli hiyo mjini Bunda.

Na: Mwandishi wetu, Bunda.

KAULIMBIU ya Jukwaa la Wazaliwa wa Mkoa wa Mara ambao wanaishi Jijini Dar es Salaam, inayowahimiza kurejea kuwekeza nyumbani, imeanza kutekelezwa wilayani Bunda.

Mmoja wa wanajukwaa hilo, Nelson Shirima tayari amejenga Hoteli ya Password mjini Bunda ambayo imezinduliwa rasmi na Mkuu wa Wilaya hiyo, Joshua Nassari aliyepongeza hatua hiyo na kualika wengine zaidi.

“Sisi kama serikali tuna encouradge(tunahamasisha) uwekezaji, tupo nyuma yenu na tupo tayari kuwasaidia kwa lolote litakalohitajika,” alisema DC.

Shirima alipongezwa pia kwa kujenga ukaribu na waendesha Pikipiki (bodaboda) pamoja na teksi, kwamba ni ubunifu ambao utamrahisishia kupata wateja.

Madereva wa bodaboda pamoja na madereva wa teksi takriban 20 walikuwa miongoni mwa wananchi waliohudhuria hafla ya uzinduzi huo, huku wakiwa wamevaa sare zenye jina na nembo ya hoteli hiyo.

Hata hivyo Nassari alimtaka Shirima kuongeza uwekezaji tofauti na hoteli, kadiri atakavyowezeshwa na Mungu na aendelee kuhamasisha ndugu, jamaa na rafiki zake wakawekeze wilayani humo.

Alisema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ipo tayari kufungua fursa za utalii maeneo mbalimbali nchini ikiwamo Bunda na kwamba ili fursa hizo zishamiri na kuleta tija lazima kuwe na maeneo ya watalii kulala kama hoteli hiyo.

Alisema uwekezaji huo unatafsiriwa kama kuunga mkono kwa vitendo, jitihada za serikali katika kukuza utalii ambazo zinachagizwa na Rais Samia kwa jitahada anazofanya katika kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika nyanja tofauti.

Naye Shirima alibainisha kuwa ingawa asili yake ni mchaga wa Rombo Mkuu, mama yake ni Mjaruo na alizaliwa na kukulia Bunda eneo la Manyamanyama kabla hajahamia jijini Dar es Salaam kikazi.

“Wana Mara Forum tuna kaulimbiu yetu kwamba wakazi wa Dar es Salaam wote ambao wametoka Mara, tuwekeze nyumbani, mimi nimetangulia nawahimiza wenzangu njooni tuwekeze nyumbani hasa wana Bunda njooni nyumbani kumenoga,” alisema Shirima.

Dhana kwamba fedha zipo kwenye majiji na mimi mikubwa, aliielezea kuwa ni dhana potofu kwasababu Mkoa wa Mara licha ya kuwa na hifadhi ya wanyama ya Serengeti ni tajiri kwa madini ya dhahabu hali inayosababisha uwapo wa migodi tofauti ukiwamo North Mara Gold Mine.

Alisema bado kunahitajika uwekezaji katika sekta ya hoteli kwamba hivi karibuni kulifanyika tamasha la Serengeti, watu walilala Mugumu na Simiyu wakati kutoka Bunda mpaka Serengeti kuna umbali kati ya km 18 hadi 25 tu.

Alitoa wito kwa yeyote mwenye nia na uwezo wa kuwekeza kufanya hivyo mkoani Mara hususan wilayani Bunda kwani licha ya kuwa katikati ya mkoa hata ofisi za TANAPA zipo wilayani humo.

Mwisho.

Previous articleRAIS SAMIA AWAZAWADIA VIWANJA TWIGA STARS
Next articleTGNP YAZUNGUMZIA MAFANIKIO MAKUBWA WALIYOPATA KUIFIKIA JAMII NA KUTATUA CHANGAMOTO ZAO.
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here