Katibu Tawala wa mkoa wa Arusha Athumani Kihamia akifungua semina ya magonjwa yasiyoambukizwa iliyotolewa kwa waandishi wa habari mkoa wa Arusha.
Meneja mpango wa Taifa wa kuzuia na kuthibiti magonjwa yasiyoambukiza Dkt Omary Ubuguyu akiongea katika semina ya waandishi wa habari mkoani Arusha juu ya magonjwa yasiyoambukizwa.
Dkt Rose Highness Mende Daktari bingwa mbobezi wa magonjwa ya Figo kutoka hosipitali ya Maunt Meru akielezea jambo juu ya magonjwa yasiyoambukizwa.
Prosper Mushi afisa lishe kutoka timu ya uendeshaji wa huduma za afya mkoa wa Arusha akieleza aina za lishe anazopaswa kula mtu ili kuufanya mwili kuwa imara na kuweza kupambana na magonjwa.
Na: Namnyak Kivuyo, ARUSHA.
Imeelezwa kuwa asilimia 33 ya watu wanafariki nchini vifo vyao vinatokana na magonjwa yasiyoambukiza ambapo magonjwa hayo yanatokana na aina ya maisha aliyoyachagua mtu.
Hayo yalielezwa na katibu tawala wa mkoa wa Arusha Dkt Athumani Kihamia wakati akifungua semina iliyotolewa kwa waandishi wa habari mkoa huo juu ya magonjwa yasiyoambukiza ambapo alisema kuwa aina ya maisha ni moja ya vitu vinavyomfanya mtu kupata kupata magonjwa au kuwa na afya njema.
Dkt Kihamia alisema kuwa semina hiyo imetolewa mahususi kwa wanahabari ili waweze kuwa chachu ya kuelimisha wananchi na kuleta mabadiliko yatayopelekea kupunguza Kasi ya magonjwa hayo.
Dkt Omary Ubuguyu meneja mpangywa taifa wa kuzuia na kuthibiti magonjwa yasiyoambukiza alisema kuwa mikoa inayoongoza kwa kuwa na watu wanaugua magonjwa yasiyoambukiza ni mkoa wa Dodoma, Arusha pamoja na Geita ambapo lengo la semina hiyo ni kuhakikisha wanatoa elimu sahihi juu ya magonjwa hayo.
Dkt Ubuguyu Alieleza kuwa limekuwa na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza jambo ambalo kwasa linapaswa kupewa kipaumbele katika kudhibiti na kupambana nayo kwani asilimia 18 ya wanaopata magonjwa hayo ni watu wenye umri chini ya miaka 30 ambapo miongoni mwa vitu vinavyochangia Ni watu kutojishughulisha, matumizi ya vilevi pamoja na kutozingatia lishe.
Dkt Rose Highness Mende daktari bingwa mbobezi wa magonjwa ya Figo kutoka hosipitali ya rufaa ya mkoa wa Arusha ya Maunt Meru alieleza kuwa magonjwa yasiyoambukiza ni magonjwa ya muda mrefu Kama vile magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, Kiharusi, Kisukari, Saratani ya shigo ya kizazi, matiti, kinywa na koo, Tezi dume, utumbo mpana, Kongosho na kuendelea.
“Magonjwa mengine ni pamoja na magonjwa ya akili, Selimundu, magonjwa ya meno na kinywa, magonjwa ya viungo, ajali zikiwemo ajali za barabarani, magonjwa yatokanayo na lishe duni Kama vile upungufu wa damu, upungufu wa vitamin A, upungufu wa madini joto, pamoja na magonjwa ya kuzaliwa nayo Kama vile vichwa vikubwa na mgongongo wazi,”Alieleza Dkt Rose.
Alifafanua kuwa magonjwa yakuzaliwa mengi yanatokana na mama kutopata lishe kamili wakati wa ujauzito, kabla na hata wakati wa ukuajia ambapo endapo juhudi za haraka hazitavhukuliwa dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza magonjwa hayo yatafikia asilimia 60 katika kusababisha vifo kwani kwa mujibu wa taarifa ya WHO watu milioni 42 Duniani kote sawa na asilimia 71 walifariki kwa magonjwa hayo.
Aidha alisema kuwa namna ya kupunguza magonjwa hayo ni kila mlo uwe na makundi yote tano ya vyakula, kula vyakula halisi kwa mfano kutokoboa, kula matunnda badala ya juice pamoja na kutoongeza sukari katika vyakula na vinywaji, namna nyingine ya kupunguza ni kutokula mafuta mengi, chumvi, kula kiasi, kujishughulisha, kutotamani vya wengine, kupata usingizi wa kutosha, kuepuka matumizi ya tumbaku na ulevi pamoja na kuchunguza afya angalau mara moja kwa mwaka.
Naye Prosper Mushi afisa lishe kutoka timu ya uendeshaji wa huduma za mkoa wa Arusha alisema kuwa lishe ni mahusiano kati ya binadamu na chakula ambapo panapokuwa na mahusiano ambayo sio mazuri kama vile kuzidisha au kupunguza ndipo madhara yanapotokea ambapo alitaja makundi ya lishe kuwa ni vyakula vya wanga, kiasi kidogo Cha sukari na mafuta, protin, mboga na matunda.
Alisisitiza kuwa kama mtu atafanya machaguo sahihi ya vyakula na kula mlo kamili pamoja na kufanya mazoezi atawezesha mwili wake kukabiliana na magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza hasa za athari za mazingira yanayosababishwa na moshi wa sigara na mionzi.