Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akizungumza na Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la NORAD Bw. Bard Vegar Solhjell walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la NORAD Bw. Bard Vegar Solhjell akimueleza jambo Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kulia kwa Mkurugenzi wa NORAD ni Balozi wa Norway nchini Tanzania Mhe. Elisabeth Jacobsen.
Kikao cha Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikino wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine na Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la NORAD Bw. Bard Vegar Solhjell kikiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto kwa Balozi Sokoine ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme akifuatilia mazungumzo hayo.
Balozi wa Norway nchini Tanzania Mhe. Elisabeth Jacobsen akielezea jambo wakati wa kikao cha Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikino wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine na Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la NORAD Bw. Bard Vegar Solhjell kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Tanzania na Shirika la Maendeleo la Norway (NORAD) zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta za nishati, utunzaji wa mazingira na matumizi bora ya ardhi.
Mkubaliano hayo yamefikiwa katika kikao kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine na Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la NORAD Bw. Bard Vegar Solhjell walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejadili maeneo ambayo NORAD imeonesha utayari wa kushirikiana na Tanzania katika kusaidia kuyaendeleza na kuyaboresha kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.
Maeneo waliyokubaliana ni nishati jadidifu, umeme vijijni, gesi asilia, elimu, matumizi bora ya ardhi, kusaidia kaya masikini, maji safi na salama, utunzaji wa mazingira na kuzuia ukataji wa miti kwa ajili ya matumizi ya mkaa na kuni pamoja na uchumi wa buluu.
Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Sokoine amemhakikishia Mkurugenzi wa NORAD Bw. Solhjell kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea na jitihada za kuhakikisha kunakuwepo na umeme wa uhakika kwa kuendelea na ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere, gesi asilia, nishati jadidifu na umeme wa jua ili kupunguza uharibifu wa mazingira kutokana na kushamiri kwa matumizi ya kuni na mkaa.
Norway imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika sekta za maendeleo tangu mwaka 1964, baadhi ya maeneo ambayo nchi hizo zimekuwa zikishirikiana ni pamoja na uzalishaji wa nishati ya umeme hususan vijijini, afya, elimu, kilimo na utunzaji wa misitu.