Benki Kuu ya Tanzania imefanya utafiti katika sekta ya benki na kubaini sababu kubwa za kuongezeka kwa mikopo chechefu ni kutokana na wafanyakazi wa baadhi ya benki na taasisi za fedha kuhusika moja kwa moja kwa kutoa mikopo bila kuzingatia taratibu, kukosa uadilifu, na kushirikiana na wakopaji katika kutoa mikopo kiuhalifu, ikiwemo vitendo vya rushwa.
Ikumbukwe kuwa kuongezeka kwa mikopo chechefu katika sekta ya benki ni moja ya sababu kubwa ya benki na taasisi za fedha kutoza viwango vikubwa vya riba za mikopo na hivyo kuhatarisha uimara wa sekta ya benki na kuathiri uchumi wa nchi.
Hivyo, Benki Kuu ya Tanzania inautaarifu umma kwamba imelazimika kuchukua hatua zifuatazo katika kudhibiti vitendo vinavyopelekea kuongezeka kwa mikopo chechefu katika sekta ya benki:
- Kuendelea kufanya ukaguzi wa benki na taasisi za fedha ili kubaini sababu za kuongezeka kwa mikopo chechefu na wafanyakazi ambao wanahusika moja kwa moja na kadhia hiyo.
- Iwapo itathibitika kuwa kuna mfanyakazi wa benki anahusika katika kutoa mikopo bila kuzingatia taratibu, kukosa uadilifu, na kushirikiana na wakopaji katika kutoa mikopo kiuhalifu, na vitendo vya rushwa, benki au taasisi ya fedha husika itatakiwa kuchukua hatua stahiki za kisheria dhidi ya mfanyakazi huyo na Benki Kuu ya Tanzania itamfungia mfanyakazi huyo kuajiriwa na benki au taasisi yoyote ya fedha inayoendesha shughuli zake nchini Tanzania;
- Kuzitaka benki na taasisi za fedha ambazo wafanyakazi wake wana mikopo chechefu katika benki au taasisi za fedha nyingine kuwasilisha taarifa zao katika taasisi za kuchakata taarifa za mikopo (credit reference bureau). Pia, Benki Kuu ya Tanzania itawazuia wafanyakazi husika kupata ajira katika benki au taasisi yoyote ya fedha inayosimamiwa na Benki Kuu, endapo itabainika kwamba kushindwa kwao kurejesha mikopo kumetokana na uzembe, uhalifu au kukosa uadilifu;
- Kuzitaka benki na taasisi za fedha kutokutoa mikopo kwa wakopaji wasio waaminifu au ambao wanakopa kwa kutumia njia za udanganyifu na kuacha kulipa. Taarifa za wakopaji wa aina hii zitatunzwa katika rejesta maalum na benki na taasisi za fedha
zitapewa orodha yao kwa lengo la kuhakikisha kuwa hawapati mikopo katika sekta ya benki. Kwa sasa, wakopaji wa aina hii wanapewa muda wa miezi mitatu, kuanzia tarehe ya taarifa hii, kufanya mipango ya kurejesha mikopo yao kabla majina yao hayajaingizwa katika rejesta maalum na benki na taasisi za fedha kupewa orodha hiyo; na
- Kuzitaka benki na taasisi za fedha kuwasilisha orodha ya wafanyakazi wa umma ambao wana mikopo chechefu ili hatua stahiki zichukuliwe. Aidha, taarifa za wakopaji kama hao nazo zitaingizwa katika rejesta maalum, na benki na taasisi za fedha zitapewa orodha yao ili kuhakikisha kwamba hawapati tena mikopo hadi hatua stahiki zimechukuliwa dhidi yao na wameanza kurejesha mikopo yao.
Benki Kuu ya Tanzania inatoa wito kwa wananchi wote ambao wana mikopo kutimiza wajibu wao wa kisheria wa kurejesha mikopo wanayokopa katika benki na taasisi za fedha. Aidha, wananchi wanahamasishwa kutoa taarifa katika benki na taasisi za fedha au Benki Kuu kuhusu vitendo vya uhalifu au rushwa wanavyokutana navyo wakati wanapohitaji huduma kutoka katika benki au taasisi ya fedha. Benki Kuu itaendelea kuwasiliana na benki na taasisi za fedha kuhakikisha taratibu za utoaji mikopo zinazingatiwa kikamilifu kwa lengo la kidhibiti kuongezeka kwa mikopo chechefu.