Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Gaudence Salim Milanzi akiongozana na Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi Balozi Edwin Rutageruka wametembelea Banda la Mamlaka ya Biashara Tanzania (TanTrade) na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) katika Maonesho ya Biashara kwa nchi za Afrika Jijini Durban Afrika Kusini.
Afisa Biashara Mkuu wa Mamlaka ya Biashara Tanzania Bw. Fortunatus Mhambe aliwaeleza umuhimu wa TanTrade kushiriki ikiwamo kujifunza kutoka kwa wataalamu wengine wa Bara la Afrika njia bora za kuhakikisha nchi za Afrika zinaongeza kasi ya kufanya Biashara kati yao.
Aidha, Bw. Fortunatus alielezea umuhimu wa Tanzania kuongeza nguvu ili kufaidika na uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara Afrika.
Kwa upande wake Balozi Milanzi aliisisitiza TanTrade kushiriki Maonesho makubwa kama haya ili kuendelea kujifunza njia mbalimbali za kuboresha Maonesho yanayofanyika Tanzania ili kufikia ubora wa Kimataifa.
Vile vile, kwa upande wake Balozi Rutageruka alipongeza juhudi zinazoendelea kufanywa na TanTrade kuhakikisha Maendeleo ya Biashara yanaimarishwa na kuhakikisha nchi inatumia vyema fursa hii ya Soko Huru kwa nchi za Afrika.