Benki Kuu ya Tanzania imetoa maelekezo kwa taasisi za fedha zinazojihusisha na biashara ya fedha za kigeni namna ya kuendesha biashara hiyo kwa lengo la kulinda utulivu wa uchumi mpana na uthabiti wa mfumo wa kifedha nchini.
Katika maelekezo hayo mapya, miamala yote ya fedha za kigeni inayozidi thamani ya Dola za Kimarekani milioni 1.0 kwa muamala mmoja katika soko la rejareja, lazima ifanyike kwa bei ya soko la fedha za kigeni baina ya benki. Aidha, miamala yote ya mteja mmoja kwa siku itajumlishwa ili kujua jumla ya kiasi husika.
Katika sekula yake kwa taasisi hizo zinazojihusisha na biashara ya fedha za kigeni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, amesema ni marufuku kufanya biashara ya fedha za kigeni na madalali wa kimataifa wa fedha za kigeni ambao hawajasajiliwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, madalali/wafanyabiashara wa fedha za kigeni hapa nchini wanatakiwa wakati wote kuzingatia utaratibu wa kumtambua mteja (KYC) kabla ya kufanya naye biashara hiyo.
Katika maelekezo hayo, kiwango cha juu cha mizania kati ya mali na amana katika fedha za kigeni (foreign exchange Net Open Position (NOP)) kitakuwa asilimia 10 ya mtaji wa msingi (core capital) na kinatakiwa kuzingatiwa wakati wote.
Ameelekeza pia kwamba Barua za Udhamini (Letters of Credit (LCs)) za shehena zinazopitia hapa nchini (transit cargoes) zitatokana na fedha za kigeni kutoka katika nchi ambako shehena hizo zinakwenda.
“Inasisitizwa kwamba uzingatiaji wa matakwa yaliyoainishwa hapa ni wa lazima na kutakuwa na usimamizi na ukaguzi kutoka Benki Kuu ya Tanzania. Kukiuka maelekezo haya kutasababisha adhabu kama zinavyoelezwa katika Sheria ya Fedha za Kigeni ya mwaka 1992,” ameeleza Gavana Tutuba.
Utekelezaji wa maelekezo ya uendeshaji wa huduma za fedha za kigeni kulingana na mahitaji ya sasa ya soko unaanza rasmi tarehe 1 Juni 2023. Aidha, maelekezo haya mapya ya tarehe 31 Mei 2023, yanafuta maagizo yaliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania tarehe 6 Agosti 2020. “Benki inawakumbusha wahusika wote wa huduma za fedha za kigeni kuzingatia matakwa ya mpango wa fedha za kigeni nchini muda wote,” ameelekeza Gavana.
Imetolewa na Idara ya Mawasiliano