Home LOCAL WATUMISHI WA AFYA KITUNDA WALALAMIKIWA KUUZA DAMU

WATUMISHI WA AFYA KITUNDA WALALAMIKIWA KUUZA DAMU

 

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora Rashid Magope (wa pili kulia) akiongea katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo jana

Na Lucas Raphael,Tabora

 

MADIWANI wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora wamesikishwa na tabia ya baadhi ya Wahudumu wa Kituo cha Afya Kitunda kilichoko wilayani humo baada ya kulalamikiwa na wananchi kuwa wanawauzia damu wagonjwa.

 

Wakiongea katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kilichofanyika jana walieleza kusikitishwa na Watumishi hao ambao hawajali maisha ya jamii kiasi cha kudiriki kuwauzia damu wagonjwa wenye uhitaji.

 

Mwalimu Peter Nzalalila, diwani wa kata ya Sikonge, akiongea kwa uchungu, alisema kuwa haingii akilini mgonjwa ambaye hajiwezi akija hospitalini hapo akiwa na upungufu wa damu anaambiwa alete hela kwanza ili aongezewe.

 

Alisisitiza kuwa jamii imekuwa ikihamasishwa kuchangia damu kwa lengo la kuwasaidia wale wote watakaokuwa na uhitaji wa huduma hiyo wakiwemo akinamama wajawazito, wagonjwa na wanaopata ajali.

 

‘Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi wa namna hii hatuwezi kuwafumbia macho,  tunaomba uchunguzi ufanyike na ikibainika kuwa malalamiko hayo yana ukweli watumishi hao wachukuliwe hatua kali za kinidhamu’, alisema. 

 

Aidha Nzalalila alisikitishwa na kitendo cha wananchi wenye Kadi za Bima ya Afya iliyoboreshwa (CHF) wanapoenda hospitalini kupata matibabu wanaambiwa dawa hamna hivyo wakanunue, alihoji huduma hiyo imeboreshwa kitu gani.

 

Diwani Yusuf Ahmed wa kata ya Kisanga alisema kuwa serikali ya awamu ya 6 ina dhamira njema ya kuboresha huduma za afya, elimu na nyinginezo lakini akasikitishwa na baadhi wa watumishi wasiozingatia maadili ya kazi zao.

 

Aliomba Ofisi ya Mkurugenzi kutofumbia macho malalamiko ya wananchi bali hatua stahiki zichukuliwe mara moja kwa wahusika pale inapobainika ukweli, vinginevyo wananchi wataendelea kuumia.

 

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Rashid Magope ambaye ni diwani wa kata ya Tutuo, alisema huduma ya damu salama inatolewa bure hospitalini na kuongeza kuwa kama kuna watu wanawauzia wagonjwa hilo ni kinyume na taratibu.

 

Alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Seleman Pandawe kuchunguza malalamiko hayo na ikibainika yana ukweli wahusika wachukuliwe hatua za kinidhamu.

 

Aidha alisema huduma ya Bima ya Afya iliyoboreshwa inasuasua, waliojiunga hawapati huduma ipasavyo, jambo linalokwamisha watu wengine kujiunga, aliagiza lifanyiwe kazi ili lisikwamishe malengo ya serikali.

 

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Seleman Pandawe alikiri kupokea malalamiko hayo na kuahidi kuwa ataunda Kamati ndogo ya kufuatilia tuhuma hizo, ikibainika zina ukweli atachukua hatua.

 

Mwisho.  

 

 


 

Previous articleMJUMITA , TFCG WABADILI MWENENDO WA WANANCHI LIWALE, WABOBEA KATIKA UHIFADHI WA MISITU
Next articleBODI YA NYAMA YAPIGA MARUFUKU MATUMIZI YA DAWA ZA KUUA NZI KWENYE MABUCHA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here