Na: WAMJW-DSM
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepokea Dozi 499,590 za Pfizer ikiwa ni mwendelezo wa mkakati wa Serikali wa kuwakinga Wananchi dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19.
Hafla fupi ya mapokezi imefanyika Novemba 23, 2021 na kuongozwa na Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na baadhi ya viongozi wa Serikali, Ubalozi na Taasisi zisizo Zakiserikali.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Gwajima amesema, Serikali kupitia Wizara ya Afya imelenga kuwakinga jumla ya Watanzania 249,795 kutokana na kupokea Chanjo dozi 499,590 za Pfizer zilizoingia kutoka Marekani kupitia mpango wa COVAX Facility.
“Leo Novemba 23, 2021 tumepokea dose 499,590 za Pfizer ambazo zitakinga watanzania 249,795 (dose mbili).” Amesema Dkt. Gwajima.
Chanjo hizi kama zilivyokuwa za Janssen na Sinopharm zimethibitishwa na WHO kuwa ni bora na salama, huku akisisitiza Wizara ya Afya itafanya wajibu wake wa kujiridhisha na uhakiki wa ubora wa Chanjo hii kwa kupitia wataalamu wa ndani na Mamlaka husika kabla ya kuanza kutolewa kwa Watanzania.
Aliendelea kusema kuwa, Hadi kufika kufikia tarehe 19.11.2021, takwimu zinaonesha kuwa jumla ya wananchi ,359,624 tayari wamepata chanjo ya kuwakinga dhidi ya UVIKO-19.
Aidha, Dkt. Gwajima amewaagiza Viongozi na Watendaji wa ngazi zote kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaelimishwa kwenda kupata chanjo ili kujikinga dhidi ya UVIKO-19.
“Ninawaagiza Viongozi na Watendaji wa ngazi za Mikoa na Halmashauri kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaelimishwa kwenda kupata chanjo ili kujikinga dhidi ya UVIKO-19. ” Amesema. Gwajima.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa huduma za Afya na Ustawi wa Jamii na Lishe OR TAMISEMI Dkt. Paul Chawote amewashukuru Wadau kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha afya ya wananchi, huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao katika kuketa Maendeleo hususan katika sekta ya afya.
Nae, Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Donald J. Wright amesema, nchi ya Marekani ndani ya kipindi cha miongo miwili imeendelea kuwa kinara katika kusaidia nchi za Afrika ikiwepo Tanzania katika kuboresha Sekta ya Afya hususan katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya UVIKO-19.
Pia, amesisitiza kuwa, hakuna muda wa kulala katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya UVIKO-19, ili kuwalinda wananchi dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO-19 ni lazima Elimu ya umuhimu wa chanjo iendelee kutolewa kisha watu wachanje. Amesema.