Home LOCAL RAIS DKT.MWINYI ATETA NA UJUMBE KUTOKA SERIKALI YA OMAN, ASISITIZA JAMBO

RAIS DKT.MWINYI ATETA NA UJUMBE KUTOKA SERIKALI YA OMAN, ASISITIZA JAMBO

 

ZANZIBAR

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amefanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje wa Oman anayeshughulikia Fedha na Utawala, Mohammed Nasser Al Wahaibi na kumueleza kwamba Zanzibar inathamini uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya pande mbili hizo.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo Ikulu jijini Zanzibar wakati Rais Dkt. Mwinyi alipokutana na Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje wa Oman anayeshughulikia Fedha na Utawala Mohammed Nasser Al Wahaibi akiwa amefuatana na ujumbe wake akiwemo Balozi wa Oman nchini Tanzania, Saud Hilal Al Shidhani.

Katika maelezo yake Rais Dkt. Mwinyi alimueleza Katibu Mkuu huyo Mohammed Nasser Al Wahaibi kwamba kwa kiasi kikubwa Oman imeweza kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya afya, elimu na mingineyo bila kusahau hatua ya nchi hiyo kusaidia ujenzi wa jengo la Beit al Jaib.

Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano huo kwa kutambua kwamba Oman ni mshirika mkubwa wa maendeleo ya Zanzibar.

Pamoja na hayo, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza haja ya kuwepo kwa ushirikiano kwa sekta binafsi kati ya pande mbili ili kuweza kutoa fursa mbalimbali za maendeleo hasa ikizingatiwa umuhimu wa sekta hiyo katika maendeleo.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi alimueleza Katibu Mkuu huyo juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwaletea maendeleo wananchi wake huku akipongeza hatua za nchi hiyo kuendelea kuziunga mkono juhudi hizo.

Naye Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje wa Oman anayeshughulikia Fedha na Utawala Mohammed Nasser Al Wahaibi alimueleza Rais Dkt. Mwinyi kwamba Oman inatambua uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na Zanzibar na kuahidi kuziendeleza kwa manufaa ya pande zote mbili.

Katibu Mkuu huyo alisema kuwa nchi ya Oman kwa kupitia Balozi zake hapa nchini zitaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza na kuimarisha sekta zake za maendeleo.

Pia, alitumia fursa hiyo kueleza umuhimu wa kuishirikisha sekta binafsi katika maendeleo jamabo ambalo limeweza ksuaidia kwa kiasi kikubwa kusukuma uchumi na medneleo nchini Oman.

Katika mazungumzo hayo, Katibu Mkuu huyo wa Mambo ya Nje wa Oman anayeshughulikia Fedha na Utawala Mohammed Nasser Al Wahaibi alizipongeza juhudi za makusudi zinazoendelea kuchukuliwa na Rais Dk. Mwinyi katika kuwaletea maendeleo endelevu wananchi wa Zanzibar.

Aidha, Katibu Mkuu huyo alimpa salamu Rais Dk. Mwinyi zilizotoka kwa Sultan wa Oman Haitham bin Tariq Al Said ikiwa ni pamoja na kueleza namna nchi hiyo itakavyoendelea kuunga mkono vipaumbele vilivyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya maendeleo ya Wazanzibari.

Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kuendelea na ziara yake kisiwani Pemba kesho Julai 25,2022 ikiwa ni pamoja na kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo inayotekelezwa kwa fedha za ahuweni ya UVIKO-19.
Previous articleWAZIRI NDALICHAKO AHIMIZA USHIRIKI WA SENSA YA WATU NA MAKAZI
Next articleRAIS SAMIA AWATAKA BODABODA KUACHA KUKWAPUA MIZIGO YATU
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here