Home LOCAL TAMISEMI YATOA ONYO KUHUSU MIUNDOMBINU, HUDUMA ZA AFYA KILWA

TAMISEMI YATOA ONYO KUHUSU MIUNDOMBINU, HUDUMA ZA AFYA KILWA

NA: OR-TAMISEMI

NAIBU Katibu Mkuu (Afya) Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Dkt. Grace Magembe amesema hajaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya unaotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa.

Amesema kuwa, Ofisi ya Rais- TAMISEMI itafanya uchunguzi wa kina katika miradi ambayo imeonekana kuwa na mapungufu na yoyote atakayebainika kurudisha nyuma utekelezaji huo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni na sheria za utumishi wa umma.

Hayo yamebainishwa tarehe 24 Julai 2022 katika ziara yake ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya katika Hospitali ya Wilaya ya Kinyonga, Kituo cha afya Hoteli tatu pamoja na Kituo cha Afya Kipindimbi zilizopo katika Halmashauri ya Kilwa.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya, kutokamilisha miradi kwa wakati ni kwenda kinyume na azma ya Serikali ya awamu ya sita ya kumsogezea mwananchi huduma bora,”amesema Dkt.Magembe.

Aidha, pamoja na ucheleshwaji huo , Dkt. Magembe ameitaka Halmashauri ya Kilwa kuzingatia maelekezo na maagizo yanayotolewa na Serikali katika utekelezaji wa miradi hasa katika matumizi ya fedha ili fedha hizo zitumike kama ilivyopangwa na Serikali.
“Ukiangalia Kituo cha Afya Kipindimbi Mil. 250 zilitakiwa zijenge jengo la wagonjwa wa nje, maabara pamoja na kichomea taka lakini kichomea taka hakijajengwa na fedha zimeisha. Hapa Hoteli tatu kichomea taka hakijajengwa, uchunguzi utakaofanyika utatuambia kwa nini mmeshindwa kutekeleza miradi hii kama Serikali ilivyoelekeza,“ amesema Dkt. Magembe.

Pamoja na hayo, Dkt. Magembe amewapongeza wananchi wa maeneo ya miradi kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuimarisha ulinzi na usimamizi wa miradi pamoja na kuchangia nguvu kazi katika utekelezaji.
Previous articleZAIDI YA BILIONI 1 ZIMEKUSANYWA KAMPENI YA GGM KILI CHALLENGE 2022
Next articleKINANA: VIJANA, WANAWAKE JITOKEZENI UCHAGUZI NDANI YA CCM TUTATENDA HAKI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here