Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (kushoto) akiongea na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe (wa pili kushoto) aliyefika ofisini kwake Sumbawanga ambapo amewataka wasaidie kutoa mrejesho wa changamoto watakazozibaini kwenye sekta ya afya ili zitafutiwe ufumbuzi.
( Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa).
RUKWA.
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe amesema wananchi wanamchango mkubwa katika kuhakikisha huduma bora za afya zinatolewa ikiwemo kujua kiwango cha fedha kinachotolewa na serikali.
Ametoa kauli hiyo leo Sumbawanga wakati alipofika kwa mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti ofisini kwake akiwa kwenye ziara ya kukagua kazi ya utoaji huduma za afya kwenye hospitali za Rukwa.
“Tupo hapa Rukwa kufanya ufuatiliaji wa utoaji huduma za afya kwenye hospitali zetu za Mkoa na Halmashauri ambapo lengo la serikali ni kuona wananchi wanapata huduma bora za afya ” alisema Dkt. Sichalwe.
Katika hatua nyingine Dkt Sichalwe amesema serikali inaendelea kuhamasisha wananchi kupata chanjo ya UVIKO-19 kwani inasaidia kuongeza kinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa huo hatari ambapo ameomba viongozi wa mkoa wa Rukwa kuendelea kutoa hamasa kwa wananchi hususan vijijni.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Joseph Mkirikiti amemtaka Mganga Mkuu huyo wa Serikali kutoa msukumo kwenye ukamilishwaji wa hospitali za Wilaya ikiwemo suala la upatikanaji vifaa tiba ili wananchi wapate huduma bora.
Mkirikiti aliongeza kusema mkoa hupokea wageni wengi wataalam lakini wanapomaliza ziara zao hawatoi mrejesho ili kuusaidia mkoa kujua yalijitokeza kwenye ufuatiliaji wao.
“Tunapokea wageni wengi toka Wizara zetu lakini hatupati mrejesho (feedback) kwani ujio wenu ni kutusaidia mikoa kujuawapi hatufanyi vema katika utoaji huduma kwa wananchi ili tuboreshe” alisema Mkirikiti.
Mganga Mkuu huyo wa Serikali yupo mkoani Rukwa kwa ziara ya kikazi itakayomfikisha wilaya ya Sumbawanga na Kalambo kukagua utoaji huduma za afya na kuzungumza na watumishi wa sekta ya afya.
Mwisho.