ARUSHA.
Wataalamu wa Ununuzi na ugavi hapa nchini wametakiwa kutumia kigezo cha kuhakiki uhalali wa kampuni zinazoomba zabuni kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA)wakati wa kufanya tathmini ya kampuni hizo.
Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa ametoa wito huo mapema leo tarehe 2 Disemba, 2021, katika mkutano wa 12 wa Wataalam wa Ununuzi na Ugavi unaoendelea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa(AICC) Jijini Arusha.
Bw. Nyaisa amesema kumekuwa na udanganyifu unaofanywa na baadhi ya kampuni zinazotaka kufanya kazi na Serikali hivyo ni muhimu kuthibitisha uhalali wake kabla ya kufanya maamuzi, hivyo ni vyema kuweka kigezo cha uthibitisho wa kampuni husika kutoka BRELA.
“Kuna baadhi ya kampuni hufunguliwa baada ya kusikia kuna kazi fulani inatafuta mzabuni hivyo kampuni za aina hiyo zinaweza kuwa na changamoto katika utendaji kazi kutokana na kutokuwa na uzoefu wa kazi husika, Wataalamu wa Ununuzi na ugavi hakikisheni kuwa kigezo cha taarifa za kampuni kutoka BRELA kinaambatishwa,” amefafanua Bw. Nyaisa.
Bw. Nyaisa amesema mbali na kupata kazi mbalimbali Serikalini kampuni zinaposajiliwa na BRELA inakuwa rahisi kupata fursa za mikopo kutoka katika mabenki kwani mabenki hufanya uchunguzi wa kampuni inayohitaji mkopo kwa kupata taarifa za kampuni husika kutoka BRELA.
Amesema mpaka sasa BRELA imekwishasajili kampuni 150,000 na mifumo ya usajili kwa njia ya mtandao inaendelea kuboreshwa ili kuondoa changamoto ndogondogo zinazojitokeza wakati wa usajili kwa njia ya mtandao.
Imeandaliwa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano.