Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul amezitaka timu za Tanzania ambazo hazikufanya vizuri katika mashindano ya Mpira wa Mikono Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati kujipanga kwa mwakani.
Kauli hiyo ameitoa leo wakati akifunga michuano hiyo iliyokuwa inafanyika katika Uwanja wa Ndani wa Taifa ,Dar Es Salaam.
Amesema kuwa serikali imelenga kuinua michezo na wameanzisha mfuko kwa ajili ya kuinua michezo hapa nchini.
“Raisi wetu mama samia amelenga kuinua michezo hivyo nawaomba sana watanzania kama leo mmeshindwa jiandae kwa ajili ya mwakani kwani kuna mfuko ambao umelenga kuinua michezo hapa nchini”amesem.
Aidha amewapongeza wachezaji na timu zilizoshiriki katika michuano hiyo na kuomba kwa umoja walioonyesha na kushirikiana katika kutafuta mshindi wa michuano hiyo.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Mikono Tanzania( TAHA) Michael Chibawala,ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa jitihada ya kuinua michezo hapa nchini.
Hata hivyo katika mashindano hayo yameshirikisha Klabu 11 kutoka nchi ya Kenya ,Rwanda na Tanzania wenyeji.
Amesema kuwa lengo ni kupata Klabu nne za juu,mbili Wanawake na mbili wanaume watakaofuzu kushiriki mashindano ya Vilabu Afrika yatakayofanyika mwakani.
“Maandalizi yapo vizuri lakini tulitarajia kuwa na Klabu 19 kutoka nchi za Afrika Mashariki na kati lakini zingine zimeshindwa kufika kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo,hivyo kwa walioshiriki tunatarajia kuona ushindani na kutimiza malengo tuliokusudia,” alisema Chibawala.
Alitaja klabu nyingine shiriki ni ya wanaume Black Mamba(Kenya)Polisi Rwanda, Ngome (Tanzania), na Nyuki (Zanzibar), huku wanawake Kizugiro(Rwanda) na Ngome(Tanzania).
Wakati huo huo mshindi wa kwanza aliibuka polisi rwanda kwa wanaume huku kwa upande wa wanawake ni Nairobi water wamepata kombe na Medali.
Nafasi ya pili imeshikiliwa Cereals wanawake na wanaume kutoka Kenya wamepata kombe na medali, huku Black Mamba wakimalizia nafasi ya tatu ,wakati upande wa wanawake Kiziguro Rwanda wamekamata nafasi ya tatu.