Na: Beatrice Sanga-MAELEZO
Serikali imesema iko katika mchakato wa kupitia Mitaala mbalimbali ya vyuo vya kati na vyuo vikuu ili kuhakikisha kwamba wanamaliza ama kupunguza tatizo la wahitimu wa Elimu ya Vyuo vya Juu pamoja na Vyuo vya kati kukosa ujuzi unaohitajika katika soko la ajira ambalo limekuwa likisababisha kupunguza uzalishaji viwandani pamoja na ushindani sokoni.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji alipokuwa akizindua Kamati ya Ushauri ya Viwanda ya Chuo Kikuu cha Mzumbe huku akiamini kwamba kamati hiyo itafanya kazi yenye tija kwa taifa.
“Tumezindua Kamati hii kupitia mradi mkubwa ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia, kamati hii iko mahususi kwaajili ya viwanda vyetu nchini kuangalia mahusiano kati ya mazao yanayotoka katika elimu ya juu na viwanda vyetu, Je, wanafunzi wanaozalishwa kutoka kwenye vyuo vyetu vikuu wanaweza kufikia mahitaji yale yaliyoko sokoni? Kwasababu kumekuwa na kilio kwa muda mrefu sasa kwamba mahitaji ya soko ni tofauti na wanaozalishwa kutoka kwenye vyuo vyetu, wanafunzi wetu hawalingani na mahitaji ya soko.” Ameeleza Dr. Kijaji.
Dr. Kijaji amesema kuwa kuzinduliwa kwa kamati hiyo kutatoa fursa kwa serikali kwenda kuangalia changamoto ya kuwepo kwa wahitimu wasio na ujuzi unaotakiwa sokoni ambayo imekuwepo kwa muda mrefu kati ya waajiri na waajiriwa huku ikitajwa kusababisha gharama kubwa kwa waajiri kuwaendeleza wahitimu hao ili kuendana na mahitaji ya uzalishaji katika maeneo yao ya kazi.
“Sasa tumeingia kwenye eneo huru la biashara Afrika mataifa yote tunakwenda kufanya biashara moja, ambalo kama Mawaziri tunajadiliana ni soko la waajiriwa (Labor Market), waajiriwa wetu wasipopikwa vizuri kule kwenye vyuo vyetu tunakuwa kwenye changamoto kubwa, sasa tutakuwa tunashindana sawa na waajiriwa kutoka maeneo mbalimbali ndani ya Afrika kwahiyo tunatakiwa tujipange, taifa linataka nini, dunia inataka nini kwenye soko la ajira ili yanayofundishwa katika vyuo vyetu yalingane na yanayohitajika sokoni.”Amesema Dkt. Kijaji
Aidha, Waziri huyo amesema kuwa vyuo vinatakiwa kupunguza upungufu uliopo wa kitalaam na kiujuzi (Skills mis-match) ili kuhakikisha wanaondoa changamoto hiyo ambayo imekuwa ikilalamikiwa kwa muda mrefu hapa nchini.
Kwa upande wake Prof. William Mwegoha Kaimu Makamu wa chuo Kikuu cha Mzumbe amesema kwa sasa Elimu ya Juu ina jukumu kubwa la kuhakikisha inafanya mageuzi katika Sekta ya Elimu kupitia mradi wa Mageuzi ya Elimu ya juu kwa Mageuzi ya uchumi (Higher Education for Economic Transformation) unaofadhiliwa na Benki ya dunia ambapo Chuo hicho kimepokea Dola za Marekani Milioni 21 kwaajili ya kutekeleza mradi huo.
“Hii kamati iliyoundwa itasaidia sana kushauri namna ambavyo tunatakiwa kuboresha mitaala tunayotakiwa kuitengeneza ili kukidhi mahitaji ya soko lakini pia kuangalia namna ambavyo tutashirikiana na watu wa viwandani, walimu wetu wanatakiwa wawe wanapata huu ujuzi tunapofundisha hawa vijana ili waweze kukidhi soko la ajira viwandani na maeneo mengine, inabidi na walimu wetu wawe na ujuzi wa kuwaandaa hawa vijana ili wakienda kule basi wakawe ni chachu ya kuendeleza vile viwanda,” amesema Prof. Mwigoha.
Aidha amesema kuwa kwa sasa vyuo havina budi kuzalisha watalaam ambao watakidhi matakwa kwenye maeneo ya fursa mbalimbali kwenye Kanda ya Afrika lakini pia kwenye masoko mengine duniani, katika maeneo ya ubunifu na ujasirimali huku pia Chuo hicho kina mpango wa kuainisha utaratibu wa kuwalea vijana wenye mawazo mazuri ambayo ni ya kijasiriamali na kibunifu ili yaweze kuendelezwa kwaajili ya mtaji wa kibiashara lakini pia yaweze kutengeneza ajira kwa vijana wa Kitanzania.
Naye Akila Bonipahce Mollel Rais wa Serikali ya wanafunzi Chuo Kikuu cha Mzumbe ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati hiyo amesema kuwa watajitahidi kutumia fursa hiyo ili kujifunza mambo mengi kutoka sekta binafsi ambayo itahusika katika kutoa mafunzo na fursa za kujifunza kwa vitendo kwa wanafunzi hao katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji.
“Tunategemea wanafunzi kunufaika zaidi na kutengenezwa ili kuendana na soko la ajira ambalo ndilo lengo haswa la sisi kuweza kusoma hata kufikia ngazi hii, lakini pia kupata ujuzi kutoka kwa watalaam mbalimbali kutoka kwenye viwanda kwa maana ya huko nje ambako watakuwa wanashirikiana na chuo chetu, kupata nafasi za kufanya mafunzo kwa vitendo kwa maana ya internship ambayo yawatawasaidia kuendelea kujifunza na kuwapa ujuzi zaidi kwenye kufanya na kutelekeza ambayo wameyasomea kwa mdua mrefu.”
Utafiti kutoka Umoja wa waajiri hapa nchini uliofanywa mwaka 2014 unaonesha kuwa mahitaji ya soko hayaendani na kinachozalishwa kwenye vyuo vikuu pamoja na vyuo vya kati hivyo kamati hii itasaidia kutatua changamoto hiyo.
Mwisho.