Mkurugenzi Mkuu wa JamiiForums, Maxence Melo (katikati) akizungumza wakati wa uzinduzi wa Shindano la Stories of Change 2023 ambalo linatarajiwa kuanza Mei 1, 2023 kwenye Ofisi za Jamii Forums, Kawe Dar es Salaam, leo Aprili 24, 2023. Kushoto ni Mwenyekiti Press Clubs Dar es Salaam (aliyewakilisha UTPC), Samson Kamalamo, kushoto ni Moses Matiko, mwakilishi kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Mwanza (SAUT) ambao ni sehemu ya wadau katika shindano la mwaka huu.
Mkurugenzi Mkuu wa JamiiForums, Maxence Melo (katikati) akifanyiwa mahojiano na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa Shindano la Stories of Change 2023 ambalo linatarajiwa kuanza Mei 1, 2023 kwenye Ofisi za Jamii Forums, Kawe Dar es Salaam, leo Aprili 24, 2023.
NA: MWANDISHI WETU
ASASI ya Kiraia ya JamiiForums (JF) imezindua msimu mpya wa Shindano la Stories of Change kwa Mwaka 2023 ambalo litafanyika kwa siku 90 kuanzia Mei 1, 2023 huku zawadi ya jumla kwa washindi watano itafika kiasi cha Tsh. Milioni 20.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, leo Aprili 24, 2023, Mkurugenzi Mkuu wa JamiiForums, Maxence Melo amesema awamu hii washiriki wataandika maudhui yanayolenga kuchochea mabadiliko chanya katika Uwajibikaji na Utawala Bora.
Amesema malengo ya shindano hilo ni kuhamasisha uandishi wa maudhui bora na yenye tija mtandaoni, kuhakikisha mtandao unabaki mahali salama ambapo umma unaweza kupata habari/taarifa bora.
Ameongeza kuwa shindano hilo linalenga kuwapa nafasi raia wote wenye uwezo wa kutayarisha maudhui, kushiriki uandishi wa maudhui mtandaoni yenye kuleta mabadiliko na mgeni rasmi katika ufunguzi wa mwaka huu wanatarajia atakuwa Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete.
Amesema Shindano la 2023, JF itashirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Mwanza (SAUT) na Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kwa kutambua mchango wao katika upashanaji Habari ikiwa ni pamoja na kushiriki katika kuwandaa wananchi/vijana waliosomea taaluma ya habari, pia kufanya tafiti mbalimbali zinazoleta mabadiliko nchini.
Kuhusu vigezo na masharti kwa washiriki, amesema: “Mshiriki anatakiwa kutayarisha andiko linalochochea mabadiliko kwenye nyanja zote za Utawala Bora (ikiwemo Uwajibikaji).
“Andiko liwe kwa Lugha ya Kiswahili lenye maneno kati ya 700 na 1,000, kuhus matumizi ya picha, vielelezo na video yanaruhusiwa ili kuongezea uzito wa wasilisho, pia ikiwa picha/video zilizotumika si za mshiriki, atatakiwa kutaja chanzo.
“Aidha, Machapisho yanatakiwa kuwa halisi ambayo hayajawahi kuchapishwa sehemu nyingine yoyote wakati ambapo Ubwakuzi (Plagiarism) haitaruhusiwa.”
Alielezea jinsi ya kushiriki, Melo amebainisha Maandiko yawasilishwe kupitia jukwaa la “Stories of Change 2023″ kwenye tofuti ya JamiiForums.com
Anasema “Mshiriki lazima awe mwanachama aliyejisajili JamiiForums.com, pia washiriki wanaweza kutumia majina yao ya kuigiza (pseudonyms) katika shindano hilo lakini mshindi atatakiwa kuwa tayari kutoa utambulisho wake halisi kwa madhumuni ya kukabidhiwa zawadi pale atakaposhinda.”
Upatikanaji wa washindi, Melo ameweka wazi kunatarajiwa kuwa na jopo la majaji linaloundwa na wataalamu 5 wenye mchango mkubwa katika masuala ya uwajibikaji na utawala bora nchini, ambapo litaamua washindi kulingana na vigezo vilivyowekwa.
“Kura za majaji zitabeba 60% ya ushindi huku kura za wananchi jukwaani zikibeba 40% ya ushindi.
“Washindi watapewa taarifa kuhusu ushindi na akaunti rasmi ya JamiiForums kupitia ujumbe wa faragha katika akaunti zao walizotumia kushiriki na kisha kutangazwa kwenye jukwaa la JamiiForums “Stories of Change” na kurasa za JF katika mitandao ya kijamii na si vinginevyo,” anasema Melo.
Shindano la Mwaka 2021 lilishirikisha wananchi 1,509 na kuandika machapisho 1,536, Mwaka 2022 lilishirikisha washiriki 1,820 waliaondika machapisho 2.
MWISHO.