Home LOCAL UPASUAJI WA KUZIBUA MSHIPA WA DAMU WA MOYO WAFANYIKA KWA NJIA YA...

UPASUAJI WA KUZIBUA MSHIPA WA DAMU WA MOYO WAFANYIKA KWA NJIA YA TIBA MTANDAO

Wataalamu wa magonjwa ya moyo na wazibuaji wa mishipa ya damu ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakimfanyia mgonjwa upasuaji  mgumu (Complex Percutaneous Coronary Intervention – PCI)  wa kuzibua mshipa wa moyo uliokuwa umeziba kwa asilimia 99 na hivyo kushindwa kupitisha damu vizuri  kwa njia ya tiba mtandao (Telemedicine). Wataalamu kutoka Shirika la madaktari Afrika waliopo Hospitali ya Central jimbo la Virginia nchini Marekani walikuwa wanatoa maelekezo ya jinsi ya kuzibua mshipa huo kwa wenzao wa JKCI waliopo nchini Tanzania.


Wataalamu wa magonjwa ya moyo na wazibuaji wa mishipa ya damu ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza kumfanyia mgonjwa upasuaji mgumu (Complex Percutaneous Coronary Intervention – PCI) wa kuzibua mshipa wa moyo uliokuwa umeziba kwa asilimia 99 na hivyo kushindwa kupitisha damu vizuri kwa njia ya tiba mtandao (Telemedicine). Wataalamu kutoka Shirika la madaktari Afrika waliopo Hospitali ya Central jimbo la Virginia nchini Marekani walikuwa wanatoa maelekezo ya jinsi ya kuzibua mshipa huo kwa wenzao wa JKCI waliopo nchini Tanzania.

Picha na JKCI

Na: Mwandishi Maalum – Dar es Salaam

Kwa mara ya kwanza wataalamu wa magonjwa ya moyo na wazibuaji wa mishipa ya damu ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamefanya upasuaji  mgumu (Complex Percutaneous Coronary Intervention – PCI)  wa kuzibua mshipa wa moyo uliokuwa umeziba kwa asilimia 99 na hivyo kushindwa kupitisha damu vizuri  kwa njia ya tiba mtandao (Telemedicine).

Upasuji huo uliochukuwa muda wa saa moja umefanyika leo kwa kutumia mtambo wa Cathlab (Catheterization Laboratory) Carto  3 System 3d & Mapping Electrophysiology  system ambapo wataalamu kutoka Shirika la madaktari Afrika waliopo Hospitali ya Central jimbo la Virginia nchini Marekani walikuwa wanatoa maelekezo ya jinsi ya kuzibua mshipa huo kwa wenzao wa JKCI waliopo nchini Tanzania.

Akizungumza mara baada ya kumaliza kufanya upasuaji huo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Peter Kisenge alisema wameweza kuzibua mshipa ambao ulikuwa umeziba kwa kiasi kikubwa kwa kufuata maelekezo ya moja kwa moja ambayo yalikuwa yanatolewa kwa njia ya mtandao wa zoom kutoka kwa  wenzao waliopo nchini Marekani.

“Tangu tumeanza kufanya upasuaji mdogo wa kuzibua mishipa ya damu kwa njia ya tundo dogo linalotobolewa kwenye paja au mkono kwa kutumia mtambo wa Cathlab mwaka 2014 Madaktari Afrika kutoka nchini Marekani ndiyo waliokuwa wanatuelekeza na kutusimamia hadi tumeweza kufanya upasuaji huu sisi wenyewe”,.

“Hata leo wametuelekeza kwa njia ya mtandao jinsi ya kufungua mshipa huu ambao ulikuwa umeziba kwa kiasi kikubwa kwani wenzetu hawa wanautaalamu mkubwa zaidi kuliko sisi . Iwapo atatokea  mgonjwa mwenye tatizo kama hili tutaweza kumfanyia upasuaji kama tulivyofanya kwa mgonjwa huyu”, alisema Dkt. Kisenge.

Mtaalamu huyo wa uzibuaji wa mishipa ya damu ya moyo alisema miaka ya nyuma  upasuaji kama huo ulikuwa unafanyika nje ya nchi, lakini kutokana na kuwepo kwa vifaa vya kisasa pamoja na wataalamu wa kutosha hivi sasa huduma kama hizo zinatolewa  hapa nchini katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

“Kama mgonjwa huyu angetibiwa nje ya nchi gharama za matibabu zingekuwa ni zaidi ya shilingi  milioni 20 lakini mgonjwa huyu ametibiwa hapa nchini kwa gharama ya shilingi milioni sita , kwa kuwa mgonjwa huyu amejisajili na mfuko wa Taifa wa bima ya afya (NHIF) gharama zote za matibabu zimelipwa na bima hii. Ninawashauri wananchi wajiunge na NHIF kwani pindi watakapoumwa watalipiwa gharama za matibabu”, alisisitiza Dkt. Kisenge.

Naye Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI Khuzeima Khanbhai ambaye alishiriki katika upasuaji huo alisema tukio hilo ni la kihistoria kwa kushirikiana na Madaktari Afrika waliopo nchini Marekani  wameweza kuzibua mshipa ulioziba kwa njia ya mtandao ingawa kuna tofauti ya muda kwao ni saa sita usiku na Tanzania ni saa moja asubuhi wamekubali kusaidia kumfanyia upasuaji mgonjwa.

“Unapofanya upasuaji wa aina hii kuna njia mbili ambazo ni mshipa wa kwenye paja au mkononi za kupitisha vifaa ili uweze kuufikia moyo”,. Kwa kuwa uzibuaji huu ulikuwa ni mgumu tulitumia njia ya kwenye paja tukapitisha vifaa na kuzibua mshipa huo, tunavyofanya upasuaji wa aina hii mgonjwa anakuwa macho tunazungumza naye  anachomwa sindano ya ganzi katika eneo husika hii inatusaidia kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na mgonjwa”,.

“Wagonjwa wenye matatizo ya kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo ni wengi kwa wiki tunachunguza na kutibu wagonjwa kati ya  50 hadi 60 na kwa mwaka huu huyu ni mgonjwa wa 1499. Kuna wagonjwa ambao wanakujakama wana  tatizo la gesi  tumboni lakini baada ya vipimo wanaonekana mishipa yao ya damu ya moyo imeziba”, anasema Dkt. Khuzeima.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi alisema wamekuwa wakifanya kambi maalum za upasuaji mdogo ambao ni mgumu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo na Madaktari Afrika waliopo nchini Marekani lakini kutokana na tatizo la Ugonjwa wa UVIKO- 19 madaktari hao wameshindwa kuja nchini.

Prof. Janabi alisema kuwepo kwa mtambo wa mpya wa Cathlab kumewasaidia  kupata maelekezo kutoka kwa wataalamu wa nje ya nchi wenye utaalamu wa juu zaidi ya jinsi ya kufanya upasuaji ambao wataalamu waliopo nchini hawawezi kuufanya.Wagonjwa wenye matatizo hayo walikuwa wanapelekwa nje ya nchi lakini kwa msaada wa wataalamu wenzao wanaweza kuwatibu wagonjwa hao hapa nchini.

“Zoezi hili limeenda vizuri na siku ya Kesho au kesho kutwa  mgonjwa atakuwa ameruhusiwa na leo hii  baada ya masaa 6 ataanza kutembea mwenyewe .  Ninaishukuru sana Serikali kwa uwekezaji mkubwa wa tiba ya magonjwa ya moyo uliofanyika katika Taasisi hii”, alishukuru Prof. Janabi.

Kwa upande wake mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji huo Mzee Owiti Wataye alishukuru kwa huduma ya matibabu aliyoipata na kusema alikuja katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) akitokea Hospitali ya rufaa ya Kanda ya Bugando akiwa na maumivu makali kwenye kifua upande wa kushoto pia shingo na mgongo vilikuwa vinamuuma sana.

“Nilikuja hapa nikiwa na maumivu makali ya kifua, shingo na mgongo  shida hii imekuwa ikinisumbua kwa muda wa miaka miwili,  baada ya kuzibuliwa mshipa  wa moyo kwa sasa najisikia vizuri ingawa bado niko kitandani lakini maumivu yamepungu kwa kiasi kikubwa”, anasema Mzee Wataye.

Previous articleABU DHABI YAAHIDI KUENDELEA KUIPIGA JEKI TANZANIA KIMAENDELEO
Next articleMIZENGO PINDA ANONGESHA MKUTANO WA WADAU WA DEMOKRASIA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here