WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan itahakikisha inaendelea kusimamia madai ya madereva pamoja na haki za waajiri katika kutekeleza madai ya madereva wa malori.
“Lengo ni kuhakikisha madereva wanaendelea na ajira zao na wanapata maslahi yao kwa mujibu wa sheria ili waweze kuendesha shughuli zao na familia zao na Serikali itasimamia madai yao na haki za waajiri katika kutekeleza madai ya madereva wasije wakawajibika na vitu ambavyo haviko kwenye sheria zetu za nchi.”
Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kukitaka Chama Cha Madereva nchini kiruhusu huduma za usafirishaji ziendelee kutolewa wakati Serikali ikiendelea kushughulikia masuala yao.
“Serikali haitaridhika kuona madereva wanalalamika kila siku na pia si vizuri waajiri wakabebeshwa mizigo iliyo nje ya sheria.
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumanne, Julai 26, 2022) wakati akizungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Innocent Bashungwa, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi pamoja na Makatibu Wakuu wa Wizara hizo na Kamishna Jenerali ya Polisi, Camilius Wambura, kwenye ukumbi wa Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma.
Katika kikao hicho ambacho pamoja na mambo mengine kililenga kujadili suala la mgomo wa madereva wa malori, Waziri Mkuu amesema awali kulikuwa na malalamiko ya madereva ambapo Serikali ilikutana na wadau wakiwemo waajiri na wamiliki wa maroli na kukubaliana masuala mbalimbali ya kutekeleza.
Amesema malalamiko ya madereva hao ni kutopewa mikataba ya kazi, kutokuwa na uhakika wa matibabu yao na familia zao (bima ya afya) na kutounganishwa katika mifuko ya hifadhi ya jamii ili wawe na uhakika wa kupata mafao baada ya kustaafu. Aidha, walidai kutopatiwa posho mbalimbali.
Pia, Waziri Mkuu amesema madereva hao wanataka kupokelea mishahara yao benki badala ya kupewa mikononi.
“Chama cha madereva kiorodheshe kampuni ambazo hazijatekeleza makubaliano baina yao na madereva badala ya kuzuia malori kutoa huduma kwani kufanya hivyo ni uhujumu uchumi.”
Waziri Mkuu amesema Serikali haipendi kuona mgogoro huo ukiendelea na kuathiri shughuli za waajiri ambao wametekeleza majukumu yao, hivyo ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani iondoe vikundi vinavyozuia madereva hao kutekeleza majukumu yao.
“Sheria zipo wahakikishe zinasimamiwa na hatua zichukuliwe kwa wanaozikiuka.” “Kama kuna dereva ambaye hajakubaliana na kampuni yake atoe taarifa kwenye chama chao na kifanye jitihada za kutatua jambo hilo na iwapo chama hicho kitashindwa kitoe taarifa Serikalini ili isaidie katika kusimamia madai yao ikiwa ni pamoja na kuona wanachodai na kumsikiliza anayedaiwa kisha kufanya maamuzi.”
Mheshimiwa Majaliwa amesisitiza usimamizi ufanyike kuhakikisha magari yote yaliyokwama katika maeneo mbalimbali nchini hususani mipakani yanaandaliwa utaratibu wa kukwamuliwa na kuendelea na safari huku masuala yao yakiendelea kutafutiwa ufumbuzi. “Usalama wa raia na mali zao usimamiwe ili watu wasipoteze mali zao.”