Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula ambaye ameambatana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel leo wamewasili Jijini Instanbul, Uturuki kwa ajili ya kushiriki kwenye Mkutano wa Tatu wa Wakuu wa Nchi wa Afrika na Uturuki (Turkey – Africa Partership Summit) na kupokelewa na Balozi wa Tanzania Nchini Uturuki Lut. Gen. Yacoub Hassan Mohamed.
Mhe Balozi Liberata MulaMula atamuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Viongozi wa Nchi unaotarajiwa kufanyika Tarehe 18 Disemba 2021 ukiwa na kauli mbiu ya Kuimarisha Ushirikiano kwa ajili ya Maendeleo.
Mkutano wa Viongozi wa Nchi utatanguliwa na Mikutano ya Mawaziri inayotarajiwa kufanyika Tarehe 17 Disemba 2021 ambayo itahusisha mkutano baina ya Mawaziri wa Mambo ya Nje, Mkutano wa Mawaziri wa Afya ambapo wataangazia uhusiano na ushirikiano baina ya Tanzania na Uturuki katika kuboresha zaidi Sekta ya Afya nchini na mapambano dhidi ya UVIKO-19.