Na: Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Shirika la Haki Yangu Foundation limeshiriki Bonanza la Michezo lililoongozwa na Kampeni ya Kataa Uhalifu Toa Taarifa Shinyanga Bila Uhalifu Inawezekana’ katika kata ya Chibe Manispaa ya Shinyanga.
Kampeni hiyo iliyoandaliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa Uratibu wa Amos John maarufu MC Mzungu Mweusi imefanyika leo Jumamosi Aprili 15,2023 katika kata ya Chibe kupitia Bonanza la Michezo lililohudhuriwa na mamia ya wananchi ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Samizi.
Akizungumza wakati wa Bonanza hilo, Afisa Programu wa Shirika la Haki Yangu Foundation bi. Christa Christian amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na serikali na wadau kutokomeza vitendo vya uhalifu katika jamii ambavyo ni pamoja na ukatili wa kijinsia.
“Uhalifu ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia. Haki Yangu Foundation tutaendelea kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali kupambana na uhalifu ili jamii iwe salama, na jamii ikiwa salama maendeleo yanakuwepo”,ameeleza Christa.
Katika hatua nyingine amesema Shirika hilo la Haki Yangu Foundation ambalo siyo la kiserikali limelenga kutetea na kuwezesha wanawake na watoto kupata maendeleo kisheria, kiuchumi,kijamii na kisiasa.
“Dira ya Haki Yangu Foundation ni kuleta maendeleo kisheria, kijamii,kiuchumi na kisiasa kwa wanawake na watoto nchini Tanzania tukiwa na dhamira ya uwezeshaji wa mafunzo na ushauri wa kisheria, kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa wanawake na watoto mijini na vijijini”,ameongeza Christa.
Bonanza hilo limehusisha utoaji elimu mbalimbali ikiwemo ya kukataa uhalifu na utoaji taarifa za uhalifu, ukatili wa kijinsia, huduma za kibenki, mashindano ya mbio za baiskeli kwa wanawake na wanaume, utoaji chanjo ya UVIKO 19, uchangiaji damu salama, ngoma, muziki, mchezo wa mpira wa miguu kati ya Radio Faraja na Chibe Combine fc na burudani kadha kadha ikiwemo onesho la Jeshi la Jadi Sungusungu kata ya Chibe.
Kwa upande wa mbio za baiskeli kwa wanawake waliozunguka uwanja wa mpita wa miguu mara 10 mshindi wa kwanza ni Temineta Charles aliyeondoka na zawadi ya shilingi 50,000/=, mshindi wa pili Grace Machiya shilingi 40,000/= ,mshindi wa tatu Happiness Ramadhani shilingi 30,000/=, mshindi wanne Dorcas Amosi shilingi 20,000/= na mshindi wa tano Elizabeth Hamis shilingi 10,000/= ambapo zawadi hizo zimetolewa na Shirika la Haki Yangu Foundation.
Akizunguza wakati wa bonanza hilo, Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Samizi amelipongeza Jeshi la Polisi Shinyanga na wadau kwa kuandaa Bonanza hilo la michezo huku akitoa wito kwa wananchi kuepuka vitendo vya uhalifu na watoe taarifa za matukio ya uhalifu ikiwemo wanaohujumu mradi wa Reli ya Mwendokasi (SGR) unaopita katika kata hiyo ya Chibe.
Mhe. Samizi ameikumbusha jamii kuhusu umuhimu wa uwabikaji wa kila mmoja katika kupiga vita mmomonyoko wa maadili katika jamii vinavyochochea matukio ya ulawiti na ubakaji akisema hayo yote yanatokea kutokana na kuwepo kwa mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Aidha amesema vitendo vya ukatili wa kijinsia vinapaswa kupingwa na kila mmoja ili jamii iwe salama kwa ajili ya maendeleo nchini huku akisisitiza wazazi kulea watoto vizuri ili kuepuka wimbi la watoto wa mitaani.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi amesema Kampeni hiyo imefanyika katika kata ya Chibe Manispaa ya Shinyanga ambayo ni miongoni mwa kata za kimkakati zinazopitiwa na Mradi wa Reli ya Mwendokasi (SGR).
Kamanda Magomi amewataka viongozi na wananchi washirikiane kutoa taarifa za uhalifu huku akikemea matukio ya baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mkononi kushambulia watuhumiwa wa uhalifu.