Home LOCAL HUDUMA ZA AFYA SIKONGE ZABORESHWA

HUDUMA ZA AFYA SIKONGE ZABORESHWA

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora Rashid Magope (mwenye suti nyeusi mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na madiwani wa halmashauri hiyo baada ya kumalizika kikao cha robo ya kwanza ya baraza la madiwani wa halmashauri hiyo. Picha na Lucas Raphae

Na: Lucas Raphael,Sikonge.

HALMASHAURI ya wilaya Sikonge Mkoani Tabora imeendelea kuboresha utoaji huduma za afya tiba na kinga katika vituo vyake vyote 37 vya kutolea huduma hizo ikiwemo maeneo ya vijijini.

Hayo yamebainishwa juzi na Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Rashid Magope alipokuwa akizungumza na Wataalamu, Watendaji na Madiwani katika kikao cha baraza kilichofanyika katika ukumbi wa Ndawkilo.

Alisema kuwa maboresho hayo yametokana na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali kwa kuwezesha ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya katika halmashauri zote nchini.

Mbali na ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya pia serikali imeleta dawa za kutosha katika halmashauri hiyo jambo ambalo limepunguza kwa kiasi kikubwa kero ya upatikanaji dawa katika zahanati, vituo vya afya na hospitali ya wilaya.

Aidha aliongeza kuwa kuanzishwa kwa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) iliyoboreshwa kumewezesha wananchi wengi zaidi wilayani humo kupata huduma za afya kwa gharama nafuu na kuepuka usumbufu uliokuwepo huko nyuma.

Magope alibainishaa hadi sasa jumla ya kaya 1,157 zimejiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) iliyoboreshwa tangu kuanzishwa kwake Januari 2019, na kuwezesha waliojiunga kupata matibabu bure kwa kipindi cha mwaka mzima.

Alisisitiza kuwa juhudi za kuhamasisha wananchi kujiunga na Mfuko huo zimeendelea kufanyika hivyo akatoa wito kwa madiwani na watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha hili linakuwa agenda katika mikutano yao yote.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Seleman Pandawe aliishukuru serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea fedha za kutosha kwa ajili ya kuboresha huduma za kijamii.

Alibainisha kuwa hadi sasa wameshapokea zaidi ya sh bil 1.5 ambazo hazikuwemo kwenye bajeti yao kwa ajili ya kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo huduma za afya na elimu.

Pandawe aliongeza kuwa huduma za afya sasa zinatolewa katika maeneo yote mjini na vijijini na hata kule ambako hakuna vituo vya afya halmashauri imeendelea kupeleka huduma hizo kupitia njia ya Mkoba.

Aidha alisema huduma ya upimaji Virusi Vya Ukimwi (VVU) imeendelea kutolewa katika vituo vyote 37 vya kutolea huduma za afya kuanzia ngazi ya zahanati, vituo vya afya na hospitali.

Diwani wa kata ya Sikonge  Peter Nzalalila alisisitiza kuwa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inafanya kazi nzuri sana, hivyo akawataka wataalamu kuwa makini sana na fedha zinazoletwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Alishauri Ofisi ya Mkurugenzi kuhakikisha huduma za afya zinatolewa kwa wananchi wote pasipo upendeleo, ikiwemo kuwachukulia hatua watumishi watakaobainika kwenda kinyume na maadili ya kazi zao.

Mwisho.

Previous articleKMC YAIPIGIA HESABU RUVU SHOOTING
Next articleWANANCHI WAHAMASIKA CHANJO YA CORONA, WAPIGA SIMU KUPATIWA CHANJO
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here