Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya barabara zinazotumika kupeleka watalii katika Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro kwa kushirikiana na wadau na mamlaka zinazohusika kwa lengo la kuwawezesha watalii wanaotembelea hifadhi hiyo kufika kwa urahisi.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Moshi Vijijini, Mhe. Prof. Patrick Ndakidemi aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuboresha barabara zote zinazowapeleka watalii mlima Kilimanjaro.
Amefafanua kuwa miongoni mwa jitihada zilizofanyika za kuboresha miundombinu ya barabara katika hifadhi hiyo ni pamoja na ujenzi wa barabara za Machame, Mweka na Marangu kwa kiwango cha lami.
Pia, amesema Serikali imeendelea kufanya ukarabati wa mara kwa mara wa barabara za changarawe zinazoelekea katika lango la Rongai, Lemosho, Kilema, Londorosi na Umbwe.
Aidha, Mhe. Masanja amesema katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali itafanya ukarabati kwa kiwango cha changarawe kwa barabara inayoelekea kwenye lango la Umbwe.