Home LOCAL AYSHAT: MSICHANA MIAKA 21 ALIYEDHAMIRIA KUJENGA KITUO KULEA YATIMA, WAISHIO MAZINGIRA MAGUMU

AYSHAT: MSICHANA MIAKA 21 ALIYEDHAMIRIA KUJENGA KITUO KULEA YATIMA, WAISHIO MAZINGIRA MAGUMU

Dar es Salaam.

Ayshat Sanya huenda likawa jina geni kwa wengi wetu, lakini kwa watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu aliowahi kuwatembelea, wanamfahamu vema.

Ni msichana mwenye umri wa miaka 21 hivi sasa, akiwa amefanikiwa kushawishi wenzake 10 kuungana naye katika kusaidia jamii.

Mitandao ya kijamii ikiwa ni sehemu ya nguzo zake anazozitumia kujenga hamasa na mtandao huo wenye mlengo chanya kwa jamii yake.

Hivi karibuni tumefanya mahojiano na Msichana huyo, pamoja na mama yake, Dk. Zaitun Bokhary. 

Karibu ufuatane nasi… “Msichana huyu mdogo alianza kuonesha mapema kwamba ana kitu ndani yake cha kupenda kusaidia yatima na wasiojiweza,” anasema Dk. Zaitun.

Dk. Zaitun ni Bingwa wa Upasuaji wa Watoto na Makamu wa Rais wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania {MEWATA}.

Anasema katika Chama chao wana desturi ya kutembelea vituo mbalimbali vya wahitaji ikiwamo yatima na kuwapa mahitaji mbalimbali.

“Ni katika shughuli hizo, kuna wakati nilikuwa naenda na Aishat, tangu akiwa na umri wa miaka mitatu.

“Ni binti yetu wa kwanza kuzaliwa, ni mtulivu, mwelevu na anayejiamini mno.

“Akiweka nia ya jambo fulani, mara nyingi hulitimiza, ana ushawishi kwa wenzake na wengi humsikiliza na kumfuata,” anasema Dk. Zaitun.

Anaongeza “Ana mvuto kwa watoto pia, kadri umri wake ulivyokwenda mapenzi yake na watoto yalizidi kuongezeka.

“Nilipokuwa nakwenda naye kule vituoni, kuna muda tulijikuta tunamtafuta, kumbe yupo katikati ya kundi la watoto, akizungumza na kucheza nao.

Anasema kuna nyakati zilikuwa ngumu kwake pale alipoketi na kuzungumza na watoto hao wa vituoni.

“Mara nyingi alikuwa akiniambia tuondoke na fulani, tumchukue na fulani twende nao nyumbani, kama tungewachukua ungekuta watoto wengi mno nyumbani kwetu.

“Nilikuwa namueleza hatuwezi kuondoka nao, tutaendelea kuwatembelea, ilikuwa nyakati ngumu, alihuzunika mno,” anasema.

Ayshat anasema hata akiwaona watoto wakiwa wakitembea-tembea kuombaomba barabarani huhisi vibaya moyoni mwake.

Anasisitiza kwamba amedhamiria kutimiza maono yake ya ujenzi kituo kikubwa cha kusaidia watoto yatima na waishio katika mazingira magumu.

Ni maono makubwa mno kulinganisha na rika lake, Ayshat anasema anaamini Mwenyezi Mungu atamuwezesha kuyatimiza kwani ni jambo jema.

“Huwa najiuliza vitu vingi, muda ambao wanaranda-randa huku na kule wenzao wako masomoni, kwanini wapo pale, nani atawasaidia, najiona jukumu hilo ni languNajua sitaweza kuwachukua wote lakini kwa sehemu kubwa nitakuwa nimesaidia jamii yangu,” anasema.

Msichana huyo amefanikiwa kuunganisha vijana wenzake wapatao 10 wanaoshirikiana katika kusaidia jamii.

“Awali nilianza na wachache, tulikuwa tunajichanga na kwenda kutembelea watoto vituoni, kuanzia Desemba, 2020 ndiyo tukawa tumefikia 10,” anasema.

“Mwanzoni ilikuwa ni marafiki tu tukishirikiana ila sasa tuna kikundi cha watu 10 ambapo kila mmoja ana jukumu lake katika kikundi.

“Nia na dhumuni letu kubwa ni kuweza kusaidia kwenye jamii wale wenye uhitaji ikiwepo watoto yatima, watoto wasio na makazi, wanafunzi mashuleni wenye mahitaji maalum.

“Kwa mfano watoto wa kike wasio na uwezo kupata taulo za kike na mahitaji mengine muhimu,” anasema.

Anaongeza “.., Pia tunatumia mitandao yetu ya kijamii ikiwamo WhatsApp, Instagram, Snapchat kupaza sauti kwa masuala yanayosumbua jamii na yanayoathiri vijana kwa njia moja au nHyingine. 

“Sisi wote {kwenye kikundi} ni wanafunzi wa vyuo mbalimbali,” anasema Ayshat ambaye hivi sasa yupo nje ya nchi akisomea masuala ya biashara.


Ayshat anawashukuru wazazi wake kwa malezi bora wanayompatia, yaliyomsaidia kujitambua.

Anawashukuru vijana wenzake waliokubali kuungana naye katika kusaidia jamii na hivi sasa wanakamilisha hatua za usajili wa Taasisi.

Dk. Zaitun anasema yeye na mumewe wamekuwa wakiwaongoza vijana hao ili watimize malengo yao.

“Huwa tunachanga pia wanapokwenda kutembelea vituo, nawapa usafiri, kwa mfano hivi karibuni walitembelea kituo kimoja huko Bagamoyo.

“Wazazi na walezi nawasihi wanapoona vijana wana maono kama haya wawasaidie waweze kuyatimiza,” anatoa rai.

Makala haya yameandaliwa na Veronica Mrema.

Credit – Matukio na Maisha Blog.

Previous articleKUTOKA MEZA YA MAGAZETI ASUBUHI YA LEO ALHAMISI DISEMBA 30-2021
Next articleIBRAHIM AJIBU AMWAGA WINO AZAM FC
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here