Home LOCAL WAJIBU YAZIPIKA AZAKI, WAANDISHI WA HABARI USIMAMIZI WA FEDHA ZA UMMA

WAJIBU YAZIPIKA AZAKI, WAANDISHI WA HABARI USIMAMIZI WA FEDHA ZA UMMA


Meneja wa Fedha na Utawala wa Taasisi ya WAJIBU, Jackson Mmary akizungumza mbele ya Wanahabari na Wadau wa Asasi za Kiraia (AZAKI) kutoka maeneo mbalimbali nchini wakati wa ufunguzi wa Mafunzo siku mbili yanayoendelea jijini Dodoma yaliyohusu namna ya kufanya uchambuzi wa masuala ya uwajibikaji na usimamizi wa fedha za umma,lengo mojawapo ikiwa ni kujengeana uwezo wa kuchambua ripoti zinazohusu uwajibikaji wa fedha za umma.

Akizungumza mbele ya wadau hao wakati wa ufunguzi wa Mafunzo hayo ya siku mbili jana Machi 29, 2023,jijini Dodoma Meneja wa Fedha na Utawala wa Taasisi ya WAJIBU, Jackson Mmary ameeleza hatua kwa hatua umuhimu wa kuwa na wadau kutoka maeneo mbalimbali ili kujengeana uwezo wa kuchambua ripoti zinazohusu uwajibikaji wa fedha za umma.

Amefafanua kuwa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu (CAG) ambayo inahusu masuala ya fedha ni nyenzo muhimu ya kufuatilia mipango ya Serikali Kuu ama Serikali za Mitaa na taasisi za kiraia.

“Tumekuwa tukifanya uchambuzi wa ripoti ya CAG peke yetu kwa kipindi cha miaka sita iliyopita, sasa tumeona kuna umuhimu wa kuwashirikisha wadau. Kwa muelekeo wa WAJIBU tukasema ukitaka kwenda haraka nenda peke yako lakini ukitaka kwenda mbali nenda na wenzako, kwa hiyo tukaona ni muda muafaka kuanza kwenda na wenzako,” amesema Mmary na kuongeza:

“Miaka iliyopita tulikuwa tunafanya uchambuzi halafu tunawaletea, sasa hivi tunataka kuwaongeza ili sisi na ninyi tufanye uchambuzi kwa pamoja halafu tukitoka hapa twende mbele. Kwa kufanya hivyo tutawezesha kujenga kwa pamoja yale tuliyokuwa tunayachambua na kuwaletea.

Kwa hiyo hivi sasa nanyi mtakuwa na uwezo wa kuchambua, kwa hiyo tutakuwa na nguvu zaidi kwa sababu ya kuhusika sote kwa pamoja. Kingine kitatuongezea mawanda ya uchambuzi kwani tumekuwa tukifanya uchambuzi kama sisi na kama tulikuwa watu 20 hapa leo wapo zaidi ya 40.”

Kutokana na uwezeshaji uliofanywa, kwa sasa amesema kutakuwa na macho mengine 80 zaidi yale yaliyokuwa yanafanya uchambuzi mwanzoni.

“Sisi WAJIBU na ninyi kuanzia leo tukitembea kwa pamoja tutakuwa tumejijengea uwezo, ninyi mtakuwa mmetujengea uwezo na sisi tunawajengea uwezo, kwa hiyo tutaongeza uzoefu na hasa ninyi mnaofanya kazi mikoani katika halmashauri.

Pia kuna mambo ambayo inawezekana tusiyaone namna ambavyo yanaathiri jamii na kila mtu anahoji ndio maana hapa kuna redio za jamii, magazeti ya kitaifa pamoja na kuna asasi za kiraia. Kwa hiyo tukiweka huo mchanganyiko tutaongeza mawanda, uzoefu zaidi katika kufanya uchambuzi wa mambo yanayoathiri jamii,” amesema Mmary.

Previous articleMAGAZETI YA LEO ALHAMISI MACHI 30,2023
Next articleMTANDAO WA MASHIRIKA YA KAIRUKI (KHEN) WAJIPAMBANUA KIMATAIFA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here