Na: Devota Mwachang’a
Mradi Bunifu wa elimu wa Shule Bora umefanikisha kuwajengea uwezo walimu zaidi ya 10,000 kwa kuwapa mafunzo kuboresha ufundishaji na umahiri katika baadhi ya mikoa unapotekelezwa mradi huo, ndani ya mwaka mmoja.
Shule Bora ni Mradi wa elimu wa serikali unaofadhiliwa na serikali ya Uingereza kupitia mfuko wa UK aid, unatekelezwa chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (MoEST) na Ofisi ya Rais – TAMISEMI katika mikoa Tisa nchini kwa msaada wa kiufundi kutoka Cambridge Education, ADD international, International Rescue Committee na Plan International.
Maelezo hayo yametolewa na Mratibu wa mradi kutoka TAMISEMI Winfrid Chilumba alipokuwa akitoa tathmini ya mwaka mmoja wa utekelezwaji wa mradi wa Shule Bora katika semina ya kuwapa uelewa wa mradi huo wahariri na waandishi wa habari iliyofanyika ukumbi wa NACTE jijini Dar es Salaam mwishoni mwa Juma.
“Mradi huu umefanikisha umekuwa chachu ya kuboresha elimu kwenye mikoa Tisa ambao walimu wengi wemepata mafunzo wakiwemo 6,937 ambao wamejifunza kuibua hadithi za mafaniko za kujifunzia za mfano ili kuboresha ujifunzaji na ufundishaji katika halmashauri 29 za mikoa ya Pwani, Katavi, Kigoma na Singida,” amesema.
Pia amebainisha kuwa jumla ya walimu
4,944 kutoka halmashauri 19 za mikoa 7 inakotekelezwa mradi wamefundishwa kuhusu miongozo ya mafunzo endelevu ya walimu kazini (MEWAKA), na wengine 944 wamepatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo katika machakato wa ufundishaji.
Amesema walimu 1,747 wa elimu ya awali, Darasa la I na la II, wawezeshaji rika na viongozi wa elimu ngazi ya Mikoa, halmashauri, kata na shule katika mikoa ya Rukwa, Pwani, Simiyu, Mara, Dodoma na Tanga nao walipewa mafunzo.
Nae Godfrey Mulongo Deputy team leader Shule Bora Programme kutoka Cambridge Education Tanzania (CETL) ameeleza kuwa kabla ya kuanza utekelezaji walianza kwa kujenga msingi wa mradi, kuhakikisha mradi wa Shule Bora unakidhi mpango kazi na vipaumbele vya serikali katika kuboresha elimu.
“Tulianza na kuweka mipango kwa kuwapatia mafunzo walimu kupitia MEWAKA kuhakikisha walimu wanatatua changamoto ya kumudu kusoma, Kuandika na kuhesabu (KKK) kwa watoto, na kuwaongezea elimu walimu ili wawaze kuwa wabobezi katika somo la Kiingereza,” amesema Mulongo.
Mradi wa Shule Bora unatekelezwa Kwa miaka Saba (2021-2027) kwenye mikoa tisa unapotekelezwa mradi wa Shule Bora ambayo ni Rukwa, Pwani, Simiyu, Mara, Dodoma, Katavi, Kigoma, Singida na Tanga, mikoa hii ilipendekezwa na TAMISEMI baada ya kugundulika haifanyi vizuri kielimu kutokana na changamoto mbakimbali zikiwemo za utoro, mdondoko wa wanafunzi, idadi hafifu ya uandikishwaji wa watoto kuanza shule.
Mwisho