Home LOCAL TUUNGANE KUTOKOMEZA KIFUA KIKUU – WAZIRI MKUU

TUUNGANE KUTOKOMEZA KIFUA KIKUU – WAZIRI MKUU

*Awataka Ma-DC wasimamie fedha za ununuzi wa dawa*

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wananchi waungane na Serikali na wadau wa maendeleo kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu na kuzuia maambukizi mapya pamoja na vifo.

“Tunahitaji kuungana na kuweka mikakati ya pamoja ya kuutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu. Iwapo kila mmoja wetu atatekeleza wajibu wake, katika mapambano dhidi ya kifua kikuu, tunaweza kukata mnyororo wa maambukizi mapya na kuzuia vifo visivyo vya lazima kwa kuwa ugonjwa huu unatibika na kupona kabisa,” amesema.

Ametoa wito huo leo mchana (Ijumaa, Machi 24, 2023) wakati akizungumza na mamia ya wananchi na wadau waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya Halmashauri ya Mji wa Bariadi, mkoani Simiyu. Pia amezindua Mkakati wa Uwajibikaji wa Pamoja wa Kisekta dhidi ya Kifua Kikuu (MAF – TB).

“Kila mmoja wetu anao wajibu wa kuhakikisha anachukua hatua zote za tahadhari kwani mgonjwa mmoja wa kifua kikuu ambaye hajagunduliwa na kuwekwa katika utaratibu wa matibabu, ana uwezo wa kuambukiza watu kati ya 10 mpaka 20 kwa mwaka. Nitoe rai kwa kila mwananchi kuzingatia maelekezo ya yanayotolewa na Wizara ya Afya na Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa katika kujilinda dhidi ya ugonjwa huu,” alisema.

Amesema mkakati uliozinduliwa leo ni takwa la kidunia na umekuja wakati muafaka ambapo Tanzania ikiwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa inatekeleza Mkakati wa Dunia wa Kutokomeza Kifua Kikuu ifikapo mwaka 2030. “Mkakati huu pia unaenda kuimarisha ushirikiano wa kisekta ambao kwa muda mrefu umekosekana kwa kutokuwepo kwa chombo au uratibu wa pamoja.”

“Ninazielekeza wizara zote zilizobainishwa katika mkakati huu ziweke vipaumbele vya kimkakati vya kupambana na ugonjwa huu ili kuyaokoa makundi yaliyo katika hatari ya kuugua kifua kikuu kama vile wachimbaji wa madini kutokana na uchimbaji usiozingatia njia sahihi za kujikinga na vumbi litokanalo na upasuaji, uchorongaji au usafirishaji wa udongo wenye madini.”

Ameitaja sababu nyingine inayochangia kuongezeka kwa maambukizi ya kifua kikuu ni ufinyu wa hewa katika sehemu za kazi au uwepo wa makazi duni na akaziagiza Halmashauri zitenge maeneo ya wazi ya wananchi kupumzikia na pia zijenge viwanja vya michezo na burudani kama njia ya kuwezesha wananchi kupata hewa safi.

Previous articleTAIFA STARS MGUU SAWA KUFUZU AFCON, YAILAZA UGANDA 1-0
Next articleTAIFA STARS MGUU SAWA KUFUZU AFCON, YAILAZA UGANDA 1-0
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here