Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amekagua ujenzi wa nyumba mpya 400 katika kijiji cha Msomera Wilayani Handeni, Mkoani Tanga watakazohamia kwa hiari wananchi kutoka Ngorongoro.
Akizungumza leo katika ziara hiyo, Mhe. Masanja amewapongeza SUMA JKT kwa kufanya kazi vizuri kuhakikisha nyumba hizo zinakamilika kwa wakati.
“Maelekezo yetu ni kwamba hadi kufikia tarehe 30 Agosti 2022 kaya zaidi ya 50 ziwe zimeletwa katika nyumba hizi na hatuna mashaka na kazi mnayoifanya” Mhe. Masanja amesisitiza.
Aidha, Mhe. Masanja ameagiza watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kukamilisha ujenzi wa kituo cha afya kwa wakati.
“Kwa kuwa Halmashauri mmepewa jukumu la kujenga kituo cha afya, kinatakiwa kikamilike ndani ya miezi minne, fanyeni kazi usiku na mchana kuhakikisha mnakamilisha.Tusingependa nyumba ziwe zimekamilika, huduma za afya ziwe bado”Mhe. Masanja amefafanua.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Siriel Mchembe amesema kuwa agenda muhimu ni kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha ujenzi wa kituo cha afya.
Kwa upande wake Operation Commander ,Luteni Kanali Edward Anthony Mwanga amesema kuwa ndani ya miezi miwili watahakikisha wanakamilisha nyumba zote na kumuahidi Naibu Waziri kuwa hadi kufikia terehe 20 Agosti 2022 familia zaidi ya 50 zitakuwa zimehamia Msomera.
Ziara hiyo ina lengo la kuangalia utekelezaji wa majukumu ya Wizara na kuangalia changamoto ili kuzipatia ufumbuzi.