NA: NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa Mkoa wa Arusha imetoa tahadhari kwa wananchi juu ya uwepo wa wimbi kubwa la matapeli ambao wamekuwa wakiwapigia simu na kujitambulisha kuwa ni maafisa wa TAKUKURU nakuwataka kufika katika Ofisi za TAKUKURU kwa kuwatishia kuwa na tuhuma za rushwa.
Tahadhari hiyo imetolewa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha James Ruge wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu (Oktoba- Desemba) ambapo aliwataka wananchi wanapopata wito huo wasitishike na kuanza kuingia makubaliano ya kutoa fedha.
“Msitishike na kuanza kuingia makubaliano ya kutoa fedha ili kumaliza suala lao pigeni simu au fikeni kwenye ofisi zetu zilizopo karibu ili kupata uhakika wa wito huo kwani ofisi yoyote ya TAKUKURU utayoenda itawawezesha kujua kama wito huo ni wakweli au la,” Alisema Ruge.
Aidha alitoa taarifa ya ufuatiliaji wa fedha shilingi bilioni 12, 555, 685,138.27 zilizotolewa kwa wilaya zote za mkoa wa Arusha na serikali kwaajili ya utoaji wa chanjo ya UVIKO-19 na ujenzi wa miundombinu kupitia mpango wa maendeleo ya Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19 (EP4R) alisema kuwa kati fedha hizo shilingi bilioni 10,730,000,000 zilinga kujenga vyumba vya madarasa 516 na milioni 244, 623,934.25 ililenga kutekeleza shughuli mbalimbali za utoaji wa chanjo ya UVIKO-19.
Alieleza kuwa milioni 891,091,204 zililenga kujenga barabara, milioni 240,000,000 zililenga kujenga mabeni matatu, milioni 30, 000,000 zililenga kujenga Maabara moja na milioni 250, 000,000 zililenga kujenga kituo cha afya.
Alifafanua kuwa TAKUKURU mkoa wa Arusha kupitia ofisi zake za wilaya ilifiatikia miradi hiyo kwanzia hatua za awali ambapo baadhi ya miradi hiyo ilibainika kutekeleza kwa kufuata sheria na baadhi kuwa na mapungufu ambapo ofisi ikitoa ushauri na maelekezo kwa mamlaka husika na hatua za marekebisho zilifanyika.
“Mapungufu hayo ni pamoja na kutofuatwa kwa ramani za ujenzi hasa madarasa, kukosewa kwa vipimo vya milango, madirisha na veranda, kutokuwa na utaratibu mzuri katika upokezi wa vifaa, udanganuifu katika makato ya Kodi ya zuio, watoa huduma kutokuwa na stakabadhi za EFD pamoja na ucheleweshwaji vibali vya ujenzi,” Alieleza Ruge.
Alifafanua kuwa kwa miradi iliyobainika kuwa na kasoro kubwa uchunguzi umeanzishwa na lengo la ufuatiliaji huo ni kuhakikisha na kujiridhisha miradi
inatekelezwa kwa kiwango kinachotakiwa na thamani ya fedha inapatikana kwenye utekelezaji wake na kuangalia endapo Kuna uvujaji , ucheleweshwaji wa makusudi wa miradi, uchepuzi wa rasilimali za mradi na iwapo jamii inashirikishwa ipasavyo katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Aidha alisema kuwa kwa kipindi cha miezi mitatu wamepokea taarifa za vitendo vya rushwa na kuzifanya uchunguzi ambapo wamepokea 198 na kati ya taarifa hizo 128 zilihusu rushwa na 70 zilihusu makosa mengine tofauti.
“Ili kufanikisha jukumu la mapambano dhidi ya rushwa tunawajibika kushirikiana na wadau mbalimbali ili kufikisha ujumbe kwa jamii na mikakati yetu ya Januari hadi machi 2022 ni kuendelea kushirikiana na wadau, kuendelea na utaratibu wa kutembelea wananchi na kusikiliza kero zinahusiana na vitendo vya rushwa, kuendelea na kazi za uzuiaji pamoja na kupokea na kufanya uchunguzi wa malalamiko,” Alieleza.
Hata hivyo amewataka wananchi kuendelea kuipa ushirikiano tasisi hiyo na serikali kwa ujumla hasa katika kufuatilia miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuhakikisha kuwa miradi hiyo inatekelezwa kwa ukamilifu na kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika.