Home Uncategorized WAZIRI MKUU APIGA MARUFUKU MATUMIZI YA KIPIMO CHA BIDOO

WAZIRI MKUU APIGA MARUFUKU MATUMIZI YA KIPIMO CHA BIDOO

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Tobias Andengenye kwa kushirikiana na SIDO wahakikishe wanaingiza sokoni vipimo rasmi vya kupimia mafuta ya mawese na kuachana na vipimo vya asili maarufu kama BIDOO ambacho kimekuwa kikiwanyonya wakulima.

Ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Februari 27, 2023) alipotembelea Viwanda vya Kukamua mafuta ya mawese, kukausha Mbegu za Michikichi na  Kiwanda cha kusindika mafuta ya mawese cha Trolle Messle, Mjini Kigoma.

Mheshimiwa Majaliwa ametoa agizo hilo baada ya mbunge wa kigoma kaskazini Assa Makanika kuomba Serikali kuagiza kuingizwa sokoni kwa vipimo vya mafuta ya Mawese badala ya kutumia vipimo vya Bidoo

“Mheshimiwa Waziri Mkuu mkulima amekuwa akipunjwa sana kutokana na matumizi ya kipimo cha Bidoo, mnunuzi anaweka maji moto kwenye dumu na linatanuka badala ya kuingiza lita 20 linaingiza lita 25 na mkulima anapewa fedha za lita 20” Amesema Mbunge huyo.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Bidoo haikubaliki na haipo kwenye sheria hivyo mfanyabiashara kutumia vipimo hivyo ni kumnyonya mkulima “haiwezekani mnunuzi alipe fedha ya lita 20 halafu unapewa lita 25 na unamlipa mkulima fedha ya lita 20, kwasababu ya kutumia kipimo cha Bidoo”

“Mkuu wa Mkoa hili ni lako wewe na wakuu wa wilaya, nendeni kwenye masoko yote yenye bidhaa ya mawese angalieni vipimo vinavyotumika, mkikuta Bidoo zikamateni na wananchi msikubali kupima mafuta kwenye Bidoo, ukiona mnunuzi ana kipimo hicho toeni taarifa”

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu ameiagiza SIDO kuendelea kubuni teknolojia nzuri na rahisi ya kukamua mafuta ya mawese ili kuwawezesha wananchi kuwa na uwezo kuzalisha mafuta mengi na bora

“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan  ameiwezesha SIDO kwa kutoa fedha ili wabuni mitambo ya kisasa ya kukamua mafuta ya mawese mpaka kwa asilimia 100 ili kuachana na teknolojia ya zamani na kumuwezesha mkulima apate mafuta mengi ili ajikwamue kiuchumi”

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa katika kuhakikisha anaipa hadhi sekta ya kilimo Rais Dkt. Samia ameongeza bajeti kwenye Wizara ya kilimo na Wizara imeweka msisitizo kwenye mazao ya kimkakati ikiwemo Chikichi “Rais wetu anataka kuona mazao haya yanaleta manufaa kwa wananchi, Wana-Kigoma msiwe na mashaka limeni Chikichi”

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia imedhamiria kukuza zao la chikichi na itaendelea kujitoa kwa ajili ya kuhakikisha zao hilo linakuwa mkombozi kwa wakulima wote.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) mpaka sasa imeidhinisha shilingi bilioni 1.4 ambazo zitakuja hapa kwa wakulima wa chikichi, shilingi milioni 353 zimetoka kwa ajili ya AMCOS tatu, lakini leo tunatoa zaidi ya shilingi milioni 118 kwa AMCOS nyingine mbili”

Previous articleGGML YASHINDA TUZO YA KIMATAIFA YA USALAMA KWA MWAKA WA 4 MFULULIZO
Next articleKATIBU MKUU DKT. YONAZI APOKELEWA RASMI OFISI YA WAZIRI MKUU AOMBA USHIRIKIANO
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here