Dkt. Kijaji ameyasema hayo Februari 8, 2023 alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya Nchini Tanzania Mhe. Manfredo Fanti katika Ofisi za Wizara, Dodoma. Aidha, Dkt. Kijaji amemshukuru Mhe. Balozi Fanti kwa ushirikiano endelevu uliopo baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuendelea kuimarika kwa Biashara kati ya Tanzania na Nchi za Umoja wa Ulaya.
Dkt. Kijaji amemueleza Mhe. Balozi Fanti kuwa maandalizi ya Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Nchi za Umoja wa Ulaya yanaendelea vizuri ambapo Kongamano hilo linaloandaliwa na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya na Sekta binafsi na linatarajiwa kufanyika tarehe 23 na 24 Februari, 2023 jijini Dar es salaam.
Dkt. Kijaji ameongeza kuwa kupitia Kongamano hilo Hati za Makubaliano mbalimbali ya Uwekezaji baina ya Tanzania na Nchi za Umoja wa Ulaya zitatiwa saini na kutakuwa na mikutano (Session) itakayohusisha Serikali na Wafanyabiashara ambapo Viongozi mbalimbali wa Serikali wanatarajiwa kuhudhuria Kongamano hilo.
Naye Mhe. Balozi Manfredo Fanti amesema kuwa ujumbe wa watu zaidi ya 600 kutoka Nchi za Umoja wa Ulaya wanatarajia kushiriki Kongamano hilo la Uwekezaji baina ya Tanzania na Nchi za Umoja wa Ulaya.
Aidha, Mhe. Balozi Fanti amesema kwa kuwa Tanzania inatekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini (MKUMBI, Mpango huo utachapishwa katika Tovuti ya Umoja wa Ulaya na Kongamano la Uwekezaji litakalofanyika Februari 23 hadi 24, 2023 litawaunganisha wafanyabiashara wa Nchi za Umoja wa Ulaya na Tanzania na kuchangia kuongezeka kwa uwekezaji baina ya Nchi hizi mbili.