Na: WAF- TANGA.
WAZIRI wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewatembelea majeruhi wa ajali iliyotokea Februari 4 katika Wilaya ya Korogwe Mkoa wa Tanga ili kuwajulia hali na kuwafariji.
Katika ziara hiyo aliyoifanya, Waziri Ummy amewapongeza wataalamu wa afya wote kwa juhudi na kujitoa katika kuwahudumia majeruhi hao ili kuhakikisha wanarudi katika hali zao za kawaida.
“Kipekee niwapongeze sana madaktari, wauguzi na watumishi wote wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Bombo ambao kwakweli wamejitahidi kutoa huduma bora,” amesema Waziri Ummy.
Sambamba na hilo, Waziri Ummy ametoa wito kwa wananchi, hasa watumiaji wa barabara kuhakikisha wanafuata sheria za usalama barabarani ili kuondokana na ajali zinazoweza kuzuilika na kupunguza idadi ya majeruhi wa ajali za barabarani.
Aidha, Waziri Ummy amesema, Serikali inaendelea kushughulikia changamoto ya upatikanaji wa madaktari bingwa, hasa madaktari bingwa wa upasuaji wa mifupa kwa watoto.
Pamoja na hayo, Waziri Ummy amesema Serikali itaendelea kuzijengea uwezo hospitali za Wilaya ikiwemo kuwa na madaktari bingwa wa upasuaji ili ziweze kutoa huduma kwa majeruhi kwa haraka pindi wanapotokea katika maeneo yao jambo litalosaidia kupunguza msongamano katika hospitali za Rufaa za mikoa.
Nae, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo ambae pia ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya dharura Dkt. Juma Ramadhan amesema, Hospitali ilipokea jumla ya majeruhi 12 ambao kati yao ni wagonjwa 2 tu wamepewa Rufaa kwenda katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Ameendelea kusema kuwa, kati ya wagonjwa hao waliopokelewa, wagonjwa wawili (2) walipoteza maisha, na wagonjwa watano (5) waliruhusiwa kotoka hospitali hapo, huku wakibaki wagonjwa watano (5) katika hospitali hiyo, wawili (2) wakiwa wakiume na watatu (3) wakike
Mwisho.